ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amefanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Wete na kushuhudia tani 9.5 za Karafuu za magendo zilizodakwa.
Karafuu hiyo yenye thamani ya Sh milioni 140 zilitarajiwa kusafirishwa kwa magendo na kukamatwa kwa ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Kaskazini Pemba vikiwemo Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) na Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) Januari 4, 2024, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Aidha, Rais Mwinyi ameagiza asilimia 80 ya mauzo ya karafuu katika soko la dunia apewe mkulima wa karafuu na asilimia 20 kwa shirika la biashara Zanzibar (ZSTC) kutumika katika uendeshaji.

Vilevile Rais Dk Mwinyi amesema karafuu iliyokuwa bora inatoka Zanzibar kwa kuitunza vizuri na kuisafisha bei yake itaendelea kuimarika duniani.

Halikadhalika amewasihi wananchi wasifanye magendo kwa maana watapata hasara kulingana na sheria za nchi, pia amesema serikali itaendelea kuongeza bei ya karafuu.