TANROADS mambo mazuri Singida

MENEJA wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Msama Msama amesema walipanga kutumia Sh.19,718,817,000 kutengeneza barabara wanazohudumia katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 na hadi Juni 2022 walikuwa wamepokea Sh. 19,893,665,000 sawa na asilimia 101.

Taarifa hiyo aliyoitoa kwenye Kikao cha 46 cha Bodi ya Barabara jana Machi 10, 2023, chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba inasema Sh. 2,015,561,000 zilitumika kulipa madeni ya Wakandarasi waliofanya kazi mbalimbali katika Mwaka wa Fedha 2020/2021.

Mhandisi Msama kupitia taarifa yake hiyo alisema Fedha zilizobakiSh.17,145,490,000 zilitumika kulipia mikataba 36 ya kazi zilizotekelezwa katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022.

“Hadi wakati wa kutoa taarifa hii (kwenye kikao 45 cha Bodi ya Barabara ya Mkoa), Sh. Bilioni 16.824 (Sh. 16, 824,335,000) zimelipwa kwa Wakandarasi kwa kazi zilizokamilika,” alisema Mhandisi huyo.

Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha 46 cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Singida wakifuatilia kikao hicho. (Picha zote na Editha Majura).

Taarifa hiyo ni sehemu ya Ajenda ya Pili ya Kikao cha 46 inayohusu kusoma na kuthibitisha muhtasari wa kikao cha 45 cha Julai 27 Mwaka 2022.

Utekelezaji wa kazi na matengenezo ya barabara imeelezwa kukamilishwa kwa asilimia 98.6 na ilitarajiwa ifikapo mwishoni mwa Julai 2022 kazi zote ziwe zimekamilishwa kwa asilimia 100.

Alitaja kazi zilizokamilishwa kwa asilimia 100 katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 kuwa ni pamoja na matengenezo ya barabara kuu, ya kawaida, ya vipindi maalum na sehemu korofi, ya madaraja kwenye barabara kuu na matengenezo ya Barabara za Mkoa.

Mhandisi Msama akiwasilisha taarifa kwenye Kikao cha 46 cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Singida.

Mhandisi Msama alisema Sh. Milioni 229  zilitumika kutengenezea kinga kwa madaraja 28 na Sh. Bilioni 1.2 zilitumika kufanya matengenezo ya makubwa ya madaraja Saba na kwamba utekelezaji wa kazi hizo umekamilika kwa madaraja matatu kati ya matano.

Habari Zifananazo

Back to top button