Tanzania, Afrika Kusini za saini hati ya makubalino
Ni ya kuboresha sekta ya afya

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeingia makubaliano na Afrika Kusini ya ushirikiano katika sekta ya afya ili kuboresha zaidi huduma za afya na ushirikiano wa pamoja katika kubadilishana uzoefu na watalaam katika sekta hiyo.
Makubaliano hayo yamefanyika kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya Afrika Kusini Dkt. Mathume Joseph Phaahla Jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Viongozi hao wamekubaliana kuwa na mpango wa utekelezaji na ufuatiliaji wa mkataba huo na kutoa taarifa kila mwaka.

“Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa na ushirikiano wa muda katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Afya, kusainiwa kwa hati hii kutachangia kuboresha ushirikiano katika sekta ya afya.”Amesema Ummy
Akifafanua Ummy amesema, nchi hizo mbili zitabadilisha wataalam wabobezi kwenye fani mbalimbali za afya, kuwezesha mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu na kubadilishana teknolojia, kuboresha upatikanaji wa dawa, chanjo na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko pamoja na dharura za Afya.
Amesema, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili utaimarisha mfumo wa huduma za rufaa kwa wagonjwa watakaohitaji matibabu nchini Afrika Kusini.

Aidha, amesema ksainiwa kwa hati hiyo ni moja ya maazimio ya Mkutano wa Pili wa mataifa mawili (Bi – National Commission – BNC) baina ya Tanzania na Afrika kusini ambapo Azimio namba 43 lilielekeza kwamba, hati ya makubaliano katika sekta ya afya isainiwe baada ya taratibu zote ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Cyril Ramaphosa wa Jamhuri ya Afrika Kusini walisisitiza umuhimu wa kutekeleza maafikiano yaliyofikiwa na kutoa mrejesho wa utekelezaji kwa wakati.
Nae, Waziri wa Afya ya Afrika Kusini, Dkt. Phaahla, amepongeza hatua ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano hayo ambayo imefanyika katika kipindi ambacho dunia nzima inakabiliwa na majanga mbalimbali ya mlipuko ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.



