Tanzania, China kushirikiana kulinda rasilimali za majini
DAR ES SALAAM: WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imetiliana saini na Chuo cha Sayansi cha China, mkataba wa makubaliano wa kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali zilizomo kwenye maji.
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Daniel Mushi amesema utiaji saini huo uliongozwa na Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China (CAS), Profesa Wang Kegiang katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Temeke Veterani mkoani Dar es Salaam.
Amesema makubaliano hayo yanatengeneza fursa nyingine ya kuendeleza utafiti na sayansi.
Amesema pia katika utiaji saini huo alipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiografia na Limnolojia ya Nanjing, Profesa Zhang Ganlin ya msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya dola za kimarekani 190,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 576.
“CAS na Taasisi ya Jiografia na Limnolojia ya Nanjing (NIGLAS) wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) katika kuendeleza utafiti wa Uvuvi, na wamefanya miradi ya pamoja mitano ambapo wametoa machapisho tisa ya Kimataifa ambayo yametuongezea muonekano kama Tafiri na kama Tanzania,
“Kufundisha wanafunzi tisa wa shahada ya Uzamili na shahada ya uzamivu, kuwezesha maabara ya utafiti za Tafiri kwa ajili ya kufanya utafiti wa viumbe maji na uvuvi katika Ziwa Tanganyika, na ukanda wa Bahari ya Hindi,” amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chuo cha Sayansi cha China, Profesa Keqiang amesema wapo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi wa Buluu, hasa kuongeza nguvu katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji katika maji chumvi, upande wa Bahari.
Ameeleza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Sayansi na Teknologia ya China kupitia NIGLAS na TAFIRI una zaidi ya miaka 15, na ulijikita zaidi kwenye maziwa makuu na majibaridi mengine nchini. Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), Dk Ismael Kimirei amesema taasisi hiyo ya China na Tafiri zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu na kutekeleza miradi mingi ya pamoja.
Amesema ugeni huu una nafasi kubwa katika kuendeleza utafiti hivyo Desemba tisa, 2023 watakwenda Kigoma ambapo Taasisi hiyo ya China imewezesha vifaa vya utafiti kwenye maabara ya Tafiri ili kuona maendeleo yake, na kuona jinsi ya kupanua wigo wa mashirikiano.