Tanzania, China kushirikiana teknolojia ya anga

WIZARA  ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeanza mazungumzo na Shirika la Sayansi na Teknolojia la Anga la China (CASC) kwa ajili ya kushirikiana katika teknolojia ya anga za juu ‘satellite’ (space technology).

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Juni 27, 2023  kwa njia ya ‘video conference’ na kushirikisha Uongozi wa Wizara akiwemo Waziri Nape Moses Nnauye.

Wengine walioshiriki ni Katibu Mkuu Mohammed alhamis Abdulla, Naibu Katibu Selestine Gervas Kakele na viongozi wengine wa Wizara na Taasisi zake  ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya TEHAMA Tanzania (ICTC) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Kwa upande wa China, mazungumzo yalihusisha ushiriki wa Mbelwa Kairuki, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China, Mwenyekiti wa Shirika CASC, Hu Zhongmin na viongozi mbalimbali wa Shirika hilo

CASC ndiye mkandarasi mkuu wa anga za juu wa Uchina ambaye amefanya majaribio kadhaa yenye mafanikio ya kupeleka parachuti ya urefu wa juu kama sehemu ya mipango ya kukusanya sampuli za asteroid na kuziwasilisha kwa usalama duniani.

Akizungumza katika mkutano huu, Nape amesema pande zote mbili zinalenga kuimarisha mashirikiano katika teknolojia ya anga ya juu na ulinzi wa taarifa za kibinafsi.

“Hii ni sehemu ya mikakati ya serikali katika kujenga na kukuza uchumi wa kidijitali ambao utatoa maisha bora kwa Watanzania kupitia TEHAMA,” amesema.

Hatua hiyo mpya imekuja kufuatia uamuzi wa China wa kupanua sera yake ya diplomasia ya anga ya juu kwa kuzikaribisha nchi mbalimbali hasa nchi za Afrika kuchangamkia fursa zinazopatikana katika uchunguzi wa anga, kuboresha sayansi na kuzalisha wanaanga wengi.

Habari Zifananazo

Back to top button