TANZANIA ipo tayari kuzalisha bidhaa za umeme za kiwango cha juu na kuhudumia Afrika na dunia kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alipotembelea kiwanda cha vifaa vya umeme cha Multi Cable Limited (MCL) kilichopo Dar es Salaam.
Dk Kijaji alifanya ziara hiyo kuona vifaa vinavyozalishwa katika viwanda vya ndani na mazingira ya watumishi ili kuboresha na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Sasa ni muda wa wazalishaji wa ndani kuingia kwenye soko la Eneo Huru la Biashara Afrika kwa kuwa bidhaa wanazozalisha zina ubora na viwango vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango nchini (TBS).
“Nimeona wapo (MCL) kwenye miradi mbalimbali wakisambaza kwa Shirika letu la Umeme (Tanesco), Wakala wa umeme vijijini (REA) wanachukua nyaya za umeme kutoka hapa, hii inamaanisha kwamba taifa letu sasa tupo tayari kuzalisha bidhaa za kwetu za kiwango cha juu,” alisema.
Alisema Tanzania ipo katika masoko ya kikanda, Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo ni lazima wahakikishe bidhaa zinafika katika masoko hayo.
“Leo (jana) nimewaelekeza wenye kiwanda hiki, tunapomaliza ziara hii, twende ofisini tukutane ili tuweze kuwaelekeza tunaingiaje kwenye Soko la Eneo Huru la Afrika,” alisema.
Alisema mwaka 2023 walikaa ofisini lakini sasa ni muda wa utekelezaji na dhamira ya serikali ni kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa zinafika katika masoko hayo na wapo tayari kuwatafutia masoko.
“Tumeona watumishi zaidi ya 1,000 ambao wapo kwenye viwanda hivi vinavyomilikiwa na wenyeji wetu hawa MCL, hizi ni jitihada kubwa na zinaonesha kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan imeweza kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji wetu wawekeze kwenye viwanda na kufanya biashara,” alisema.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Kampuni ya MCL, Kassmary Ahmed alisema wanatengeneza vifaa vyote vya umeme ikiwamo transifoma, mita, nyaya tangu mwaka 2002.
Alisema wamefurahia ujio wa waziri wa viwanda kwani lengo lao ni kuongeza ajira kwa vijana na kuinua uchumi wa taifa.
“Tunaungana na wizara katika kukuza, uboreshaji na kuongeza ubora wa bidhaa wanazozalisha. Kampuni hii pia inajihusisha na masuala ya kijamii,” alisema.