“Tanzania imepiga jeki uchumi nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara”

DAR ES SALAAM: TANZANIA imekua kitovu cha uwekezaji na kusababisha ukuaji wa uchumi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 5.0 mwaka 2023.

Hayo yamesemwa leo Februari 27,2024 na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango na kwamba matarajio ya ukuaji uchumi kwa mwaka 2024 yakiwa asilimia 5.5

katika Jukwaa la Uwekezaji na Kodi 2024 lililofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa ya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Advertisement

Dk Mpango amesema serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera na kanuni ili kujibu changamoto za uwekezaji na wafanyabiashara ili waweze kulipa kodi kwa hiari na kuiwezesha serikali kutekeleza mahitaji kwa umma.

Amesema Serikali imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi imepaisha makusanyo ya mapato yaliyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na hiyo ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei uliofikia asilimia 3.2 kwa mwezi Julai hadi Desemba 2023 kiwango ambacho kipo ndani ya lengo la kati ya asilimia 3 hadi 7.

“Makusanyo ya Sh trilioni 22.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yalipelekea kuongezwa kwa bajeti kuu ya serikali kutoka Sh trilioni 36 mwaka 2021/2022 hadi Sh trilioni 44.4 mwaka 2023/2024 ambazo zimesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa ya SGR ambayo imefanyiwa majaribio ya mafanikio jana, ukarabati wa miundombinu ya bahari na maziwa makuu, pamoja na asilimia 79 ya vijijini kufikiwa na huduma ya maji.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele katika masuala ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuweka mazingira wezeshi na katika sera za kodi serikali imekuwa ikielekeza kukusanya kodi kwa weledi, kutoa elimu, kusimamia sera ya ulipaji kodi na usajili wa walipa kodi mpya.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF,) Raphael Maganga amesema; sekta binafsi nchini inatambua jitihada za Serikali katika kuboresha uchumi, kutambua mchango wa TPSF na kuitangaza nchi kimataifa kwa manufaa ya wananchi.