Tanzania inaongoza kwa kesi Mahakama Afrika 

RAIS wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud amesema mahakama hiyo imepiga hatua ya kiutendaji ambayo maamuzi yake yamekuwa yakitumiwa na nchi wananchama wa Umoja wa Afrika kubadili mifumo yake ya haki za binadamu.

Pia ameitaja Tanzania kuwa ni nchi inayotumia ipasavyo mahakama hiyo kutokana na zaidi ya asilimia 50 ya kesi zilizoamuliwa kutoka nchini humo.

Aliyasema hayo jijini hapa jana wakati wa kikao cha faragha kilichowakutanisha majaji wa nchi za Umoja wa Afrika chenye lengo la kutathimini utendaji kazi wa mahakama hiyo katika mashauri mbalimbali.

Advertisement

Alisema kwa sasa nchi 34 kati ya 55 wanachama wa Umoja wa Afrika zimeridhia mkataba ulioanzisha kuwa maamuzi ya msingi yaliyoletwa na mahakama hiyo yamefuatwa na nchi wanachama wa umoja huo.

“Kuna kesi tumezitolea maamuzi ya msingi maelekezo ambazo ni 150 hadi sasa, lazima tuelewe kwamba maamuzi ya hii mahakama yanatoa miongozo kwamba uvunjaji wa haki za binadamu wa namna hii haimaanishi ni kwa nchi ile tu bali inatakiwa kufuatwa na nchi zote za Afrika,” alisema.

Aidha, Aboud alisema kesi ambazo zimetolewa maamuzi ya msingi na maelekezo madogo katika mahakama hiyo ni 150 ambapo zaidi ya asilimia 50 zimetoka nchini Tanzania.

“Tanzania ni kati ya nchi ambazo zaidi ya asilimia 50 kesi zinazosikilizwa na mahakama hii zinatoka huko kabla haijatoa tamko la kuzia wananchi wake kupeleka kesi katika mahakama hiyo,” alieleza.

Alisema Tanzania haijajitoa katika mahakama hiyo na kuwa mkataba wa kuridhia kuanzishwa kwake bado upo hai.

“Na bado inagharamia mahakama hii ambayo makao makuu yake yako Arusha na ni nchi pekee ilikubali kuwa wenyeji.

“Ilitoa tamko la kuwaruhusu wananchi kuleta kesi zao mahakamani, kwa hiyo kesi nyingi sana ni za Tanzania na zilizoamuliwa ni za hapa nchini na bado zimebaki chache ambazo tunaendelea kuzitolea maamuzia” alisema Jaji Aboud.

Akizungumzia mafanikio ya kikao cha kwanza cha faragha kilichowakutanisha wataalamu wa Mahakama hiyo alisema kumekuwa na matokeo chanya ya ufanisi wa mahakama hiyo.

Alisema kikao kilichoanza jana kinalengo la kuangalia wapi mahakama hiyo imefanya vizuri, wapi kuna changamoto na namna ya kuzitatua na kama utendaji kazi unaenda sawa, au kuna mahali panatakiwa kufanyiwa marekebisho.

Kwa upande wa Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Modibo Sacko alieleza kuwa wanashirikiana na Tanzania kama nchi mwanachama ili kuhakikisha lengo la kuanzishwa kwake linatimia na kila nchi inapata inachohitaji kupitia mahakama hiyo.

Naye, Msajili wa Mahakama hiyo, Dk Robert Eno alisema kwa kiasi kikubwa Tanzania imepiga hatua kuitumia mahakama hiyo na kwamba mafanikio makubwa yamepatikana katika mahakama hiyo kiutendaji.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *