Tanzania kimbilio matibabu ya kibingwa kitaifa, kimataifa 

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini.

Huduma hizo ni za upasuaji mgumu wa moyo bila kufungua kifua, upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo, upandikizaji figo, upandikizaji uloto, upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa watoto, kuweka puto tumboni na upasuaji mgumu wa mifupa na mishipa ya fahamu.

 

Advertisement

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya katika kipindi cha miaka mitatu, huduma za ubingwa bobezi zilizotolewa ni pamoja na upandikizaji vifaa vya usikivu kwa watoto ambapo watoto 25 waliwekewa kati ya hao 11 wamewekewa vifaa hivyo mwaka 2023/2024.

Upandikizaji wa figo ulifanyika kwa wagonjwa 27, kati yao 16 wamefanyiwa mwaka 2023/2024, upandikizaji uloto wagonjwa 15 walipatiwa huduma hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2021, upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo wagonjwa 5,954 kati yao 2,289 wamefanyiwa mwaka 2023/2024.

Mengine ni wagonjwa 662 kuwekewa goti bandia, kati yao 385 wamefanyiwa mwaka 2023/2024, wagonjwa 166 wamewekewa puto tumboni tangu huduma hiyo ianzishwe mwaka 2021.

Huduma hizi zilitolewa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na hospitali nyingine za rufaa za kanda na mikoa.

Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia kuimarisha huduma za ubingwa na ubingwa bobezi umewezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo ndani ya nchi kwa gharama nafuu badala ya kuzitafuta nje ya nchi.

Aidha, uwekezaji huu umevutia wagonjwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuifanya Tanzania kuwa Kituo cha Tiba Utalii kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Tiba Utalii yang’aa

Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma za kibingwa na bobezi, Tanzania imevutia wagonjwa kutoka nje ya nchi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema kwa mwaka 2023, idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi wa utalii wa tiba waliokuja kutibiwa nchini ilikuwa 6,931 ikilinganishwa na wagonjwa 3,957 mwaka 2022 na wagonjwa 75 mwaka 2021.

Anasema wagonjwa hao wanatoka katika nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Congo DR, Uganda, Zimbabwe na Kenya.

“Wagonjwa hawa walihudumiwa katika hospitali sita ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean road, JKCI, MOI na hospitali binafsi za Aga Khan na Saifee.”

Aidha, Serikali ya Rais Samia kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi na wananchi.

“Kupitia mafunzo elekezi kutoka kwa wataalamu bingwa (Mentorship Program) kutasaidia kuleta chachu ya mabadiliko ya utoaji huduma za afya kuhudumia vyema wananchi wapate huduma bora za kibingwa.

JKCI yapata wagonjwa nje ya Afrika

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge anasema serikali imenunua mtambo mkubwa ambao haupo Afrika Mashariki na Kati kwa Sh bilioni saba ambao umeongeza wigo wa tiba utalii.

Anasema wagonjwa waliotibiwa kutoka nje ya nchi walikuwa 316 hususani kwa nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Visiwa vya Comoro, Msumbiji, Nigeria, Siera Leone, Zimbabwe, Zambia, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ethiopia na Burundi kwa nchi za Afrika.

“Tunapata watalii (wa matibabu) karibu nchi 20 ni jambo kubwa kwa sababu tumeanza kupata kutoka Ujerumani, Ufaransa, Italia na Poland wamekuja kufanya utalii na wakipata matatizo ya moyo walikuwa wanarudi kwao sasa wanakuja moja kwa moja kwenye taasisi.

“Zaidi ya mashirika 20 yanakuja kwenye taasisi yetu wanavutiwa na vifaa vilivyowekwa na rasilimali watu wanaona wakifanya huduma wagonjwa watapona wanatoka mataifa mbalimbali kwa sababu ya Dk Samia amefanya mapinduzi makubwa,” anasema Dk Kisenge.

Anafafanua Rais Samia alitoa fedha nyingi kuwekeza katika elimu kwenye vyuo vya ndani kama JKCI kuanzisha programu kwa kushirikiana na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ambapo hivi sasa wamejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pia kwa kozi za upasuaji wa moyo, tundu dogo na nesi.

“Muhas wanatoa kozi ya udaktari bingwa wa upasuaji wa moyo, karibu shilingi bilioni tisa zimetolewa kwa ajili ya mafunzo ya ndani na nje ya nchi na kuna wanafunzi wako nje ya nchi serikali inawalipia ada.

Dk Kisenge anasema huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Dk Samia Outreach Services zimetolewa katika mikoa 12 ambapo watu 10,807 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo, kati yao 4,375 walikutwa na matatizo ya moyo na kuanzishiwa matibabu na wagonjwa 1,323 waliokutwa na matatizo walipewa rufaa kwenda JKCI.

Anasema si tu wagojwa kuja ndani ya nchi lakini pia wataalamu wa JKCI walikwenda Zambia na Malawi kuwahudumia wagonjwa 731.

Ocean Road

Kwa upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Ummy anasema ilitibu wagonjwa kutoka nje ambapo kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 wagonjwa 176 walihudumiwa ikilinganishwa na 162 mwaka 2021/22.

Wagonjwa hao walitoka nchi za Kenya, Uganda, DRC, Zambia na Comoro.

 

Aidha, wagonjwa 152 kutoka Kenya, DRC, Malawi, Msumbiji, Sudan Kusini, Zambia na Uganda walipatiwa huduma za uchunguzi na tiba ya saratani nchini ikilinganishwa na wagonjwa 148 mwaka 2021/22.