Tanzania kinara utekelezaji mpango anwani za makazi
WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema Tanzania imetajwa kinara wa utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi barani Afrika kwa zaidi ya asilimia 95.
Mratibu wa Anwani za Makazi Kitaifa kutoka Wizara hiyo, Mhandisi Jampyon Mbugi amesema hayo wakati wa utoaji wa mafunzo kwa wenyeviti wa serikali za mitaa, watendaji wa kata na wa mitaa wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Washiriki wengine walikuwa ni wakusanya taarifa katika zoezi la uhakiki wa taarifa za anwani za makazi wa manispaa hiyo.
Mhandisi Mbugi amesema mafanikio hayo yanatokana na oparesheni anwani ya makazi iliyofanyika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzinduliwa kwake Februari 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan na utekelezaji kufanyika kwa njia ya operesheni iliyofikia tamati Mei 2022.
Anwani za makazi ni mfumo unaotambulisha mahali halisi ambapo mtu anaishi mahali ilipo biashara yake au ofisi anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mtaa, namba ya nyumba au jengo pamoja na Postikodi.
Mhandizi Mbugi amesema utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi barani Afrika uliasisiwa tangu mwaka 2010 na ulipaswa kukamilika mwaka 2015.
Amesema kutokana na changamoto mbalimbali zoezi hilo lilitekelezwa kwa asilimia mbili pekee na baadae kupanda kwa asilimia moja mwaka 2021.
“Tanzania baada ya serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani na kuanzisha oparesheni hiyo zoezi hili limefanikiwa kwa kiwango kikubwa ambapo kwa sasa maeneo mengi yamefikiwa.” amesema Mhandisi Mbugi
Amesema serikali iliweka msukumo katika utekelezaji na ilipofika Mei mwaka 2022 Tanzania ikawa imefikisha zaidi ya asilimia 95 na kuwa kinara barani Afrika.
Amesema, kufanikiwa kwa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi kusaidia kwa kiasi kikubwa nchi ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kidigitali.
Mhandisi Mbugi amesema hatua hiyo ni baada ya kukamilika kwa miundombinu ya utambuzi ambayo itasaidia urahisishaji wa huduma ikiwemo ufikishaji wa barua majumbani
Kwa upande wake Ofisa Tawala Wilaya ya Morogoro ,Hilary Sagala akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya mkuu wa wilaya amewataka washiriki kutekeleza zoezi la ukusanyaji wa taarifa kwa weledi kwa kuzingatia kanuni za utumishi wa umma ili kufikia malengo tarajiwa.
Amesema baada ya mafunzo hayo serikali haitasita kuwachukulia hatua baadhi ya watu watakaokwamisha zoezi hilo kwa namna moja ama nyingine.
Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanatambulika kwenye mfumo wa anwani za makazi ili kusadia kuwaletea maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.
Pia ametoa onyo kwa wananchi watakaobanika kuhujumu miundombinu ya anwani za makazi kwa kuvunja au kung’oa vibao ya majiana ya mitaa , watu hao watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
“Ni jukumu la kila mwananchi kulinda, kuitunza na kuitumia vema miundombinu ya anwani za makazi na Postikodi kwa kutambua na kuthamini umuhimu wake wa kuwezesha uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na Serikali kwa maendeleo ya Taifa letu” amesema Sagala
Dhana nzima ya uwekaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi nchini licha ya kuwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 inayotaka nchi kuwa na Anwani za Kitaifa zitakazowezesha ufikishaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi, pia ni maelekezo ya Kimataifa ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU) pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 – 2025.