Tanzania kuanzisha minada ya madini

WAZIRI wa Madini, Dk Doto Biteko amesema wanatarajia kuanzisha minada ya madini kwa lengo la kupata wanunuzi wakubwa wa kimataifa ili waje kununua madini hayo kwa bei kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.
Dk Biteko aliyasema hayo jana Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara wakati akikagua maendeleo ya Kitalu C na ujenzi wa Tanzanite Centre.
“Rais amekubali tuanzishe utaratibu wa kutafuta wanunuzi wakubwa wa madini waje ili mawe kidogo mnayopata yapate thamani kubwa kuliko ilivyo sasa na tumepata mwekezaji mpya anaitwa Franone ambapo kwa kipindi cha miezi sita amezalisha ajira 328,” alisema.
Alisema utaratibu wa kufanya biashara ya madini ndani ya ukuta ni biashara huru na kuwataka wafanyabiashara wa madini ndani ya ukuta kuuza mawe yao kwa mtu wanayemtaka bila kusumbuliwa lakini pia jiwe linalotoka ndani ya ukuta lazima lihesabiwe na kujulikana thamani yake na sehemu linapokwenda.
Naye Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopha Ole Sendeka, alimpongeza Dk Biteko kwa kuleta utulivu kwenye sekta ya madini na kumuomba aendelee kuwa balozi katika kuendeleza utulivu kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mirerani, Bernard Msengi alisema kwa mwaka wa fedha 2022/23 ofisi yake imekusanya kiasi cha Sh bilioni 2.6 sawa na asilimia 52.23 ya lengo la makusanyo huku akieleza sababu zilizosababisha baadhi ya malengo kutofikiwa ni pamoja na hali ya kijiolojia ya mashapo kuwa katika kina kirefu hivyo migodi mingi kutumia muda mrefu kufanya utanuzi na uwekezaji wa migodi pamoja na ukosefu wa teknolojia za kisasa kwa wachimbaji wadogo ndani ya eneo la ukuta.



