DAR ES SALAAM: Tanzania iko mbioni kuokoa zaidi ya Sh Bilioni 4 zinazotumika kuagiza viuatilifu vya kilimo kutoka nje ya nchi baada ya kiwanda cha Shirika la Maendeleo nchini NDC kupitia kiwanda cha uzalishaji wa viuatilifu vya kibaiolojia kuanza uzalishaji wa viuatilifu hivyo.
Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Viwanda vya Kuongeza Thamani Ester Mwaigomoli amesema Tanzania inaagiza viuatilifu hivyo kutoka nje jambo ambalo linaligharimu taifa fedha nyingi za kigeni.
“Sekta hii ya matunda na mboga mboga imekuwa sana inaajiri takribani wananchi milioni 4.4 na nchi inaagiza viuatilifu takribani lita laki mbili na nusu kwa mwaka.
“Kiwanda chetu kimetoa ‘solution’ ya kupunguza kuagiza viuatilifu hivi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni” – amesema Mwaigomoli
Nae mtaalamu wa maabara kutoka chuo hicho kilichopo chini ya NDC Jovin Magayane amesema serikali iliwekeza katika kiwanda hicho baada ya kuona zaidi ya asilimia 40 ya mazao yanayolimwa yanaharibika kutokana na wadudu waharibifu huku magonjwa ya mimea yakiigharimu serikali pesa nyingi.
“Magonjwa ya mimea yanagharimu zaidi ya sh trillioni 100 kwa hiyo unaweza kuona ni namna gani uchumi unaweza kuporomoka kutoka na wadudu waharibifu kwa hiyo kupitia kampuni hii ya TPBL kampuni tanzu ya NDC imekuja na dawa hizi za kibaolojia za kupambana na wadudu hao, ” amesema Magayane
Nao wananchi ambao ni wakulima wa mboga mboga wa eneo hilo wameishukuru NDC kwa kuwapatia suluhisho la kutotumia kemikali kuzalisha mboga hizo ili kuepusha madhara kwao na kwa walaji wa mboga hizo.
Kiwanda hicho ambacho ni cha kwanza Afrika kwa sasa kinazalisha dawa ya kuua wadudu wa kilimo kwa kutumia bakteria rafiki wa ardhini iitwayo Thurisave – 24 huku kikitarajia kujitanua zaidi.