TANZANIA inatarajia kupokea msaada wa dola za Marekani milioni 15 (takribani Sh bilioni 34.9) kutoka Shirika la Kimarekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Taasisi ya Vodafone kuwezesha usafiri wa dharura kwa wajawazito.
Kwa mujibu wa Ubalozi wa Marekani nchini, USAID na Vodafone Foundation wameahidi kutoa Dola za Marekani milioni 15 kuwezesha hilo zikiwamo Dola milioni 10 zinatolewa na Vodafone Foundation na Dola milioni tano zinazotolewa na USAID.
Ahadi hiyo ilitolewa katika kikao cha pembezoni cha Mkutano Mkuu wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaoendelea New York, Marekani.
Katika kikao hicho chini ya uenyekiti wa Mtendaji Mkuu wa USAID, Samantha Power, Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Vodafone, Joachim Reiter aliwasilisha ahadi ya kampuni hiyo kutoa fedha hizo kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha tiba nchini.
Akimwakilisha Rais Samia katika mkutano huo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alishukuru kwa msaada huo.
Dk Mpango alisema nchini takribani wanawake 4,000 na watoto 65,000 hufariki dunia kila mwaka, huku kuchelewa kupata huduma za dharura ikiwa ni pamoja na usafiri wa dharura kukichangia sehemu ya vifo hivyo.
Katika mkutano huo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema mradi huo utaisaidia Tanzania kufikia malengo iliyojiwekea katika Mkakati wa Tano wa Afya na Mpango Mkakati wa Tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ambayo moja ya vipaumbele ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto na hivyo ni chachu ya kuiwezesha nchi kufikia malengo endelevu ya kidunia.
Taarifa ya Ubalozi wa Marekani nchini ilieleza kuwa Serikali ya Tanzania imeahidi kugharimia gharama za usafiri na kutoa wahudumu wa afya tangu siku ya kwanza ya utekelezaji wa programu hiyo.
Kama sehemu ya programu ya mwaka 2013-2020 ya kusaidia afya ya wajawazito katika wilaya za Sengerema na Shinyanga, taasisi hizo mbili zilianzisha utaratibu wa wanawake wajawazito kuchangia usafiri wa bure.
“Jitihada hizi mpya zitapanua wigo wa programu hii kutoka wilaya mbili, zenye wakazi milioni moja hadi nchi nzima ya Tanzania yenye wakazi milioni 60,” ilieleza taarifa ya ubalozi huo.
Vodafone Foundation imeahidi kutoa kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni tano ili kuanzisha utaratibu huo katika nchi nyingine za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zenye kiwango kikubwa cha vifo vya wajawazito hivyo kufanya jumla ya kiasi itakachotoa kufikia Dola za Marekani milioni 15.
“USAID itaangalia uwezekano wa kuwa na programu nyingine za ubia na Vodafone Foundation ili kupeleka mafanikio yaliyopatikana Tanzania mahali pengine,” ilieleza taarifa hiyo.