Tanzania kutawala usafiri majini EAC

TANZANIA itaendelea kutawala fursa za usafiri wa majini katika nchi za Afrika Mashariki kupitia maziwa makuu ya Tanganyika na Victoria kutokana na mradi wa ujenzi wa meli unaoendelea na ukarabati wa nyingine kuwa katika hatua za mwisho.

Aidha, serikali inatarajia kuanza ujenzi wa meli mpya tatu pamoja na chelezo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alibainisha hayo jana katika Hotuba ya Bajeti ya wizara hiyo.

Alisema katika huduma za uchukuzi kupitia maziwa makuu mwaka 2022/23, Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imeendelea kutoa huduma za uchukuzi na usafiri katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa hivyo kutumia vizuri fursa za kiuchumi katika maziwa hayo.

Waziri Mbarawa alibainisha kuwa, MSCL inatekeleza mradi wa ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza (Hapa Kazi Tu) yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na kwamba, ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 83.

Alisema utekelezaji wa mradi wa ukarabati mkubwa wa meli ya Mv Umoja yenye uwezo wa kubeba tani 1,200 za mizigo umefikia asilimia 75.

8.

Meli hiyo hufanya safari zake kati ya Tanzania na nchi jirani za Kenya na Uganda kupitia Ziwa Victoria.

Kuhusu ukarabati mkubwa wa meli ya Mv Sangara katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma, alisema meli hiyo ina uwezo wa kubeba lita za mafuta 400,000 na hufanya safari zake kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia. Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 90.7.

Aidha, Mbarawa alisema serikali kupitia MSCL ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na mkandarasi kuwezesha kuanza ujenzi wa meli mpya tatu na chelezo.

“Kati ya meli hizo, mbili ambazo ni meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 na meli ya abiria na mizigo yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo zitajengwa katika Ziwa Tanganyika,” alisema.

Akaongeza: “Meli moja ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mabehewa ya mizigo itajengwa katika Ziwa Victoria na chelezo itajengwa katika Ziwa Tanganyika.”

Alibainisha kuwa Machi 5, mwaka huu MSCL ilikamilisha taratibu za zabuni kumpata mkandarasi wa ukarabati wa meli ya Mv Liemba na sasa majadiliano na mkandarasi yanaendelea kabla ya kusaini mkataba huo Julai, mwaka huu.

Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Aprili, 2023 MSCL ilisafirisha abiria 170,137 ikilinganishwa na abiria 143,468 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22 huku tani za mizigo 18,909 zikisafirishwa ikilinganishwa na tani 12,354 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22.

Alisema kuwa MSCL inakamilisha taratibu za kuajiri mhandisi mshauri kufanya tathmini na kuishauri serikali kuhusu ukarabati wa meli ya Mv Mwongozo iliyosimamishwa kazi kutokana na changamoto ya msawazo. Kazi hiyo inatarajiwa kuanza Juni na kukamilika Novemba, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button