TANZANIA kwa kushirikiana na kampuni ya VIATRIS itapata fursa ya uwekezaji katika ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa ikiwemo dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs).
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe amesema hayo leo alipofanya mazungumzo na mkurugenzi wa kampuni hiyo wa Kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Prashant Despanande kuhusu fursa za uwekezaji.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema Mkurugenzi wa VIATRIS amehahidi kuja Tanzania kwa ajili ya kufanya tathmini ambayo itawezesha utekelezaji wa kusudio hilo.
Aidha amesema kuwa uwekezaji wa viwanda vikubwa kama VIATRIS utaiwezesha Tanzania kuwa na upatikanaji wa bidhaa za afya kwa urahisi na kwa gharama nafuu pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa watanzania.
“Hatua hii itaiwezesha Tanzania kuwa na mkakati endelevu katika mwitikio wa mapambano dhidi ya UKIMWI.” Alisema Naibu Waziri.
VIATRIS ni Kampuni ya kutengeneza dawa na vifaa tiba vya afya ikiwemo dawa za kufubaza VVU.