RAIS Samia Suluhu Hassan ameahidi kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi kwa kuwa nchi hizo ni ndugu wa damu.
Rais Samia aliyasema hayo mjini Lilongwe jana kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 59 ya Uhuru wa nchi hiyo.
Rais Samia alisema ni jambo la kupongezwa kwa Malawi tangu imepata uhuru miaka 59 iliyopita wamekuwa na amani jambo ambalo ndio msingi wa maendeleo ya uchumi.
“Kama tunavyofahamu mapambano ya kupigania uhuru hayaishi mpaka mtakapopata uhuru wa kisiasa ambao pia ndio mwanzo wa ukombozi wa kiuchumi,” alisema Samia.
“Kama jirani zenu, uhuru wenu pia (Malawi) unatukamilisha sisi (Tanzania) maana tusingejihisi tuna uhuru kama jirani zetu Malawi bado wapo chini ya utawala wa kikoloni,” alisema.
Rais Samia alisema Tanzania inafurahia kuona Malawi inakuwa na kuahidi kuisapoti akiahidi kutokuwa kikwazo kwenye mafanikio yao kiuchumi.
“Tanzania na Malawi ni ndugu wa damu, majirani, tunafanana kwenye tamaduni zetu, tunakula chakula cha aina moja watu wa Malawi na wale wa Nyasa Tanzania ni wamoja,” alisema.
Alisema ndio maana hakukataa mwaliko wa kuhudhuria sherehe hizo kutokana na undugu uliopo baina ya nchi hizo. “Malawi ni nyumbani pia, mimi ni Mmalawi mwenzenu,” alisema.
“Pongezi kwako rais (Lazarus Chakwera- Rais wa Malawi) na wananchi wako, Tanzania inakuhakikishia kuwa itasimama nanyi muda wote wakati wa shida na raha,” alisema Rais Samia.
Akizungumzia changamoto za kibiashara kati ya Malawi na Tanzania, Rais Samia alisema zote zitafanyiwa ufumbuzi na ni wajibu wao kama viongozi kuhakikisha mambo yanakuwa sawa baina ya wananchi wao.
“Tangu ulipotembelea Tanzania (Rais Chakwera) Oktoba mwaka 2022 mambo mengi yamefanyika…tunahitaji kufanya jitihada zaidi kutatua suala la bidhaa na huduma kwa watu wetu ili kukuza uchumi wetu,” alisema.
Alisema tofauti zilizokuwepo kati ya nchi hizo zilishajadiliwa na pande zote zilikubaliana kufanya kazi pamoja na hana shaka mambo yanakwenda kama walivyokubaliana.
“Tutaendelea kushirikiana… ushirikiano mzuri uliopo kati yetu unanifanya kujiamini zaidi kwamba hakuna changamoto zitakazojitokeza… kwa pamoja tutafikisha nchi zetu kwenye mafanikio,” alisema.
Kauli ya Rais Samia kuhusu kuimarisha ushirikiano iliungwa mkono na Rais Chakwera ambaye pia alimshukuru Samia kwa kukubali mwaliko wake.
“Inanipa furaha kwa Rais (Samia) kushiriki nasi katika sherehe hizi, mimi na wananchi wa Malawi tumefurahi sana,” alisema Chakwera.
Tanzania na Malawi zimekuwa kwenye mgogoro wa mara kwa mara kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa ambapo awali Malawi ilidai ziwa lote ni mali yake.
Hata hivyo, mgogoro huo ulimalizwa kwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili, ingawa pia kwa siku za karibuni kumekuwa na mgogoro wa wafanyabiashara mpakani mwa nchi hizo ambao hata hivyo pia ulitatuliwa.
Rais Samia aliwahi kugusia suala la wafanyabiashara kufuata masharti katika nchi wanazokwenda ili kuepuka kero na changamoto ambazo zinaweza kuzuilika.
“Wakati mwingine unatuma watu mpakani kufuatilia mgogoro uliopo, majibu unayopata unaona aibu, unaweza kukuta mtu kaingia mpakani hana kibali, bidhaa zinazuiliwa anaanza upya taratibu mpaka akimaliza mizigo aliyobeba imeshaharibika,” alisema.
Malawi ilipata uhuru wake mwaka 1964 chini ya Utawala wa Uingereza.