DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili kwa kushirikiana na Taasisi ya Weill Cornell Medicine ya nchini Marekani wameanzisha mpango maalumu wa matibabu ya wagonjwa wa kiharusi wataofikishwa Muhimbili ndani ya Saa 24.
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof Mohamed Janabi amesema mpango huo utakuwa na manufaa makubwa kwakuwa Muhimbili inavifaa tiba vya kisasa vya kuhudumia wagonjwa wa kiharusi ikiwemo mtambo wa Angio-Suite ambao unatumika kufanya uchunguzi na matibabu ya kiharusi.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Radiolojia, Dk. Fredrick Lyimo amesema matibabu ya mgonjwa wa kiharusi yanahusisha jopo la wataalamu wengi kuanzia pale anapokelewa mpaka kupatiwa matibabu.
Lyimo ameongeza kuwa wataalamu hao watatembelea maeneo mbalimbali ambayo yanatumika kutoa huduma kwa wagonjwa wa kiharusi.
“Kwa sasa watatembelea maeneo ya kutolea huduma kuangali mtiririko mzima wa kuhudumia wagonjwa wa kiharusi kwakuwa matibabu ya kiharusi yanahusisha wataalamu wengi ikiwemo madaktari wa mishipa ya fahamu, wataalamu wa kufanya vipimo vya radiolojia, kupiga picha na kusoma majibu”amesema Lyimo
Makubaliano hayo yameingiwa baada ya wataalamu wa taasisi hiyo ya Weill Cornell Medicine kufanya mazungumzo na, Prof Janabi leo Novemba 21, 2023 ambapo pia walipata fursa ya kutembelea Idara ya Magonjwa ya Dharura na Idara ya Radiolojia ambapo wameangalia baadhi ya mashine za uchunguzi ikiwa ni pamoja na ANGIO-SUITE, MRI, X-RAY NA CT-SCAN.