KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kushirikiana na Kampuni ya Mbolea ya Serikali ya Morocco (OCP), wamesaini makubaliano ya kujenga viwanda vidogo vya kuchanganyia mbolea ili iendane na afya ya udongo hivyo kuleta tija kwenye kilimo.
Aidha, katika makubaliano hayo, OPC wataingiza nchini mbolea za kupandia, kukuzia na zile zenye virutubisho na TFC watakuwa wasambazaji wao. Hayo yamebainishwa Dar es Salaam jana kwenye mkutano wa kampuni hizo na waandishi wa habari kuhusu kufikia kwao makubaliano hayo yaliyoanza kujadiliwa mwaka 2016.
Akizungumzia kuafikiwa huko, Meneja Mkuu wa TFC, Samuel Mshote alisema hayo ni matokeo ya mkutano wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na viongozi wa mataifa hayo kuhusu kuimarisha sekta ya kilimo. “OCP ni Kampuni ya Serikali ya Morocco ambayo inazalisha mbolea katika mataifa mbalimbali na wako tayari kuleta mitambo ya kujenga viwanda zaidi ya vitano hapa nchini vya mbolea iliyochanganywa ili iendane na afya udongo wa maeneo ya wakulima wetu,” alisema Mshote.
Alisema tayari OCP imeshaingiza nchini tani 100,000 za mbolea aina ya DAP na zitasambazwa kwa wakulima. Aidha, alisema OCP wako tayari kujenga viwanda vya kati kutengeneza mbolea ya mboji itokanayo na taka zinazozalishwa katika majiji nchini na hiyo itakuwa fursa ya kuongeza ajira na upatikanaji wa mbolea.
“Kwa kawaida taka zinatumia siku 100 kuoza kugeuka mbolea ya mboji, lakini hawa OCP wako tayari kutoa mafunzo jinsi ya kutengeneza mbolea hiyo baada ya saa tatu na sio siku 100,” alibainisha Mshote. Akizungumzia makubaliano hayo, Makamu wa Rais wa OCP Ukanda wa Afrika Mashariki, Youssef Lahmiti alisema ni ya kuzalisha mbolea nchini inayoendana na afya ya udongo wa maeneo husika ili kuleta tija kwa wakulima.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dk Hussein Mohamed Omar alisema Ajenda ya Kilimo 2030 ni kwamba sekta hiyo ichangie asilimia 10 ya uchumi, hivyo matumizi sahihi ya mbolea ni moja ya vitu muhimu kufikia lengo hilo.
“Tunataka kupitia kilimo tutengeneze ajira zaidi ya 3,000, lakini pia tunataka wadau waone fursa kwenye kutengeneza mbolea ya mboji kupitia taka tunazozalisha mitaani,” alisema Dk Omar.
Akizungumza mahitaji ya mbolea nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Stephan Ngailo alisema kwa mwaka 2022/2023 mahitaji yalikuwa tani 667,000 na mwaka ujao mahitaji ni tani 800,000. Aidha, alisema upatikanaji wa mbolea umeimarika, na hadi kufika Aprili 30, 2023 upatikanaji ulikuwa tani 830,000.