Tanzania mwenyeji mkutano muziki Afrika

MKUTANO wa Music In Africa wenye lengo la kudumisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kutumbuiza (ACCES), umepangwa kufanyika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 24 hadi 26 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Music In Africa, Eddie Hatitye, akizungumza leo Novemba 4, jijini Dar es Salaam, anasema nafasi za upendeleo zitatolewa zaidi kwa wanamuziki wa Kitanzania kama washiriki wenyeji, ili kuonesha ubora wa muziki wa Kitanzania na kuwatangaza kimataifa.

Hatitye, amesema lengo kubwa la mkutano huo ni kuwajengea uwezo wasanii wa Afrika hususani Tanzania, ili waweze kutumia vipawa vyao vya muziki katika kupata fedha nyingi kama walivyo wasanii wa Ulaya.

“Kwenye muziki kuna hela nyingi, lakini  wanamuziki wa Afrika wengi wana majina, lakini hawana pesa,  wanatakiwa kujua namna ya kupata pesa, namna ya kuingia mikataba mbalimbali, ambayo haitawaumiza, namna ya kujenga mahusiano na namna ya kutumia mitandao ya kijamii ili kupata masoko ya kimataifa, hii ndio lengo hasa la mkutano la mkutano huu,” amesema.

Mkutano huo wa ACCES, hufanyika kila mwaka kwenye miji mbalimbali ndani ya Afrika, na kutoa fursa kwa wanamuziki kukuza na kujengea uwezo wao na kutumbuiza mbele ya hadhira iliyosheheni wageni wa kitaifa na kimataifa, ikiwemo waandaaji wa matamasha, mapromota, mawakala wa muziki, lebo za kurekodi muziki na wadau mbalimbali wa muziki.

Pia unahusisha warsha mbalimbali za mafunzo, mazungumzo ya kitasnia, maelezo muhimu kupitia risala, maonesho ya moja kwa moja (mbashara), vikao vya kukuza umoja na mwasiliano, kurekodi nyimbo kwa pamoja na matembezi mbalimbali kwenye vituo muhimu vya tasnia ya muziki.

“ACCES inatoa nafasi za kushiriki kwa wanamuziki wanaoibuka wenye uwezo wa kutumbuiza moja kwa moja katika majukwaa na wenye utayari wa kutumbuiza katika majukwaa ya kimataifa. ACCES inahitaji washiriki walio tayari kunufaika kupitia mkutano huo kwa kukuza kazi zao kufikia hadhi za kimataifa,” anasema Hatitye.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hassan Abbasi, akizungumzia mkutano huo, amesema wasanii wengi wa ndani wamekuwa wakilalamika kukosa fursa serikali imesikia kilio chao na kudhamini mkutano huo, mkubwa wa kimataifa ambao unashirikisha lebo kubwa za kimataifa kama Universal, Sonny na Boom Play.

“Nitashangaa mkutano huu unafanyika hapa halafu kuna wasanii watajifungie huko hawatashiriki, mpaka sasa wasanii 60 wameshajisajili kushiriki 30 wanatoka nje na 30 wa ndani, idadi hii bado ni ndogo wasanii wetu mjisajili hii ni nafasi pekee kwenu kujitangaza na kupata soko,” amesema Abbasi.

Kwa upande wa Katibu wa Shirikisho la Muziki Tanzania (TMF), Fareed Kubanda maarufu ‘Fid Q’, amesema mkutano huo wa Access, upo kwa ajili ya kukuza ‘brand’ za wasanii, ndio maana  wanafanya semina elekezi kwa wasanii namna ya kufanya bishara yao, kupata elimu katika sekta ya muziki.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button