Tanzania na Japan pamoja kuendeleza kilimo
SERIKALI ya Japan kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) hasa katika sekta ya Kilimo na usindikaji wa mazao ya vyakula ikiwa ni moja ya sehemu ya kilimo kinachofanyika nchini humo.
Balozi wa Japan nchini , Yashushi Misawa ameyasema hayo wakati wa makabidhiano ya vitabu Vitabu 61 vya lugha ya Kingereza kwa Menejimeti ya Chuo Kikuu hicho kwenye Kamapsi ya Edward Moringe.
Lengo la vitabu hivyo ni kuwasaidia Watafiti, Wasomi na Wanafunzi ili kukuza uelewa kwa Wataalamu na wasio Wataalamu katika kuchangia maendeleo ya Rasilimali watu.
Misawa amesema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni moja ya Vyuo Vikuu vyenye matumaini makubwa nchini Tanzania kutokana na ushirikiano wa karibu na nchi yake ambao umendelea kudumu kwa muda mrefu.
Amesema anaamini kupitia vitabu hivyo wataenda kupata wanafunzi kutoka chuoni hapo, vilevile nchi yao inaweza kushirikiana vizuri na SUA hasa katika Sekta ya Kilimo na Usindikaji wa vyakula kama moja ya sehemu ya kilimo ambayo hata wao wamekuwa wakiufanya.
‘‘Tumetoa Vitabu kwa Taasisi Zaidi ya 1,100 kote Ulimwenguni hadi sasa na , kwa Tanzania kwa SUA kinakuwa ni Chuo Kikuu cha nne kupatiwa vitabu baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dodoma (UDOM) , UDOM na DUCE” amesema Balozi Misawa
Naye Makamu wa Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda amesema ziara ya Balozi huyo katika Chuo Kikuu hicho ni katika kuendeleza mashirikiano baina yao ambayo yamekuwepo tangu miaka ya 70 na yamekuwa yakiendelea kuimarika siku hadi siku.