UJUMBE wa Tanzania uliopo ziarani nchini Qatar umekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Hamad Medical Corporation (HMC) Jijini Doha, Qatar ikiwa ni jitihada za kutafuta fursa mbalimbali za ajira kwenye sekta ya afya.
Ujumbe huo wa serikali uliongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab umejadiliana namna ya kuanza kutoa nafasi za ajira kwa watanzania.
Watalaam wa sekta ya Afya nchini Tanzania walikuwa hawajaanza kuingia kwenye soko la ajira la Qatar na hivyo endapo Tanzania itafunguliwa nafasi hizo itaweza kupeleka watalaamu wake kufanya kazi nchini humo.
Mkurugenzi Mtendaji Msaidizi, Idara ya Rasilimali Watu wa wa Hamad Medical Corporation, Bi. Sabeeha Amin Qasemi amesema kuwa hospitali hiyo imefurahishwa na hatua ambazo Tanzania inazichukua katika kuboresha sekta ya afya na kuahidi kuwa watatoa nafasi za ajira kwa wataalamu wa afya ambao hatimaye watapelekwa kwenye hospitali mbalimbali nchini Qatar.
Prof. Katundu ameuhakikishia uongozi wa Shirika hilo kuwa Tanzania ina wataalamu wa afya wenye uwezo na uzoefu wa kutosha na endapo watapata fursa za ajira nchini humo watafanya kazi kwa bidii na weledi kwa kuzingatia sheria na taratibu za Qatar kwa kuwa watahiniwa hao hupatiwa mafunzo wakati na baada ya usaili wa ajira.
Balozi Fatma Rajab amesema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Qatar ili kuiwezesha Serikali hiyo kupata wafanyakazi bora zaidi katika sekta mbalimbali.