Tanzania, Rwanda kukuza biashara

Tanzania, Rwanda kukuza biashara

TANZANIA na Rwanda zimekubaliana kushirikiana katika maeneo kadhaa ikiwemo kukuza biashara baina ya nchi hizo hasa baada ya kubainika kuwa kiwango cha biashara katika nchi hizo hakiendani na rasilimali za nchi hizo.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu aliyozungumza na Rais wa Rwanda, Paul Kagame Ikulu, Dar es Salaam.

“Ziara hii imetupa muda mzuri wa kutathmini masuala yote ya ushirikiano kati ya nchi zetu mbili na kubuni mbinu mpya za mashirikiano zaidi,” alisema Rais Samia.

Advertisement

Alisema katika mazungumzo yao ya ndani viongozi hao walijadili na kukubaliana kuwa kuna haja ya kukuza biashara na kuweka miundombinu ya kukuza biashara kwa sababu kiwango cha biashara kilichopo hakiendani na rasilimali zilizopo katika nchi hizo ukizingatia uhusiano mzuri uliopo.

Rais Samia alimweleza Rais Kagame kuwa Tanzania inaimarisha bandari zake hususani za Dar es Salaam na Tanga ambazo nchi hiyo inazitumia.

“Lakini pia tumezungumza kuangalia na kuimarisha njia nyingine za mawasiliano ili Tanzania itoe huduma kwa ufanisi kule Rwanda na nchi nyingine zinazotuzunguka,” alisema.

Rais Samia alisema pia waligusia suala la mradi wa umeme wa Rusumo ambao unakwenda vizuri na wamekubaliana kuwa watauzindua pamoja.

Aidha, alisema walizungumzia masuala ya ulinzi na usalama na kukubaliana vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hizo viendelee kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha usalama kwa nchi hizo lakini pia ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Rais Samia alisema katika mazungumzo yao kuna masuala waliyogusia ambao yapo tayari yamefanyiwa kazi na mengine bado na wameagiza Tume ya kudumu ya Ushirikiano na Tume ya kufuatilia utekelezaji wa yale ambayo hayajamalizwa zikutane haraka nchini.

Alizitaka tume hizo kukubaliana na kuandaa tafrija ya kusaini makubaliano hayo na kazi ziendelee.

Rais Kagame alisema Tanzania ni nchi muhimu kwa Rwanda hasa kuhusiana na usafirishaji na uunganishaji wa biashara.

“Tunashukuru nia ya Tanzania ya kuimarisha zaidi uhusiano huu kwa manufaa ya pande zote mbili, kuwezesha watu wetu kujiendeleza kwa kasi na kampuni zetu kushindana vyema katika soko la kimataifa,” alisema Kagame.

Alisema yeye na Rais Samia wamefanya mazungumzo yenye kujenga na kwamba wamejitolea kujenga uhusiano thabiti wa kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kihistoria.

Alisema urafiki na ushirikiano wa Rwanda na Tanzania umeota mizizi katika azma ya pamoja ya kuboresha maisha ya wananchi wake.

Aidha, alimshukuru Rais Samia kwa uongozi wake katika kutafuta suluhu ya migogoro iliyopo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hasa mgogoro ambao umekuwa ukishughulikiwa wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na wanachama wengine wa jumuiya hiyo.

“Kujenga amani na usalama wa kudumu katika eneo letu kutahitaji kujitolea kutoka kwetu sote wakiwemo wale walioathirika moja kwa moja na migogoro hii,” alisema Rais Kagame na akasema amani na utulivu ni hitaji muhimu kwa ajili ya maendeleo na Umoja wa Afrika.

Marais hao wote kwa nyakati tofauti walisema ziara hiyo ya Rais Kagame na kuwa fupi lakini ni ya manufaa na mafanikio makubwa kwa raia wa Tanzania na Rwanda.

Rais Kagame aliwasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jana saa saba mchana kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alimpokea kiongozi huyo na ujumbe wake na wakaenda Ikulu.

Katika mapokezi hayo, Dk Tax alifuatana na viongozi kadhaa akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu- Zanzibar, Jamal Kassim Ali, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Wengine waliokuwa katika mapokezi hayo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Samwel Shelukindo, Balozi wa Rwanda nchini, Meja Jenerali Charles Karamba na viongozi waandamizi wa serikali.

Imeandikwa na Halima Mlacha na Ikunda Erick.