Tanzania sasa kuingiza bidhaa 10 soko la Afrika

WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imesema Tanzania inapaswa kuongeza kasi na kuwa na mikakati ya kuzitumia fursa katika Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) na kwingineko duniani.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Ashatu Kijaji alisema dunia na Afrika wanaitazama Tanzania kuwa ni nchi yenye uwezo wa kuzalisha bidhaa za kilimo ziuzwe barani Afrika na duniani kwa ujumla.

“Soko la Afrika ni muhimu sana kwa nchi zetu na sasa masharti yamepunguzwa, hili lingependa sana Watanzania tuelewane, masharti yamepunguzwa, tumeambiwa tupeleke bila ushuru kwa kiasi chochote, nchi zote 54 za bara hili zinaongea hii lugha, tusipoanza sisi kupeleka wao wataleta,” alisema Dk Kijaji.

Alisema kuna haja ya kujiuliza Tanzania inawezaje kuitumia ardhi nzuri iliyonayo ili nchi inufaike kwenye AfCFTA kwa kuuza bidhaa zenye ubora.

Dk Kijaji alisema hayo Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wadau wa biashara kujadili na kupanga mikakati ya kuzitumia fursa za soko kwenye eneo huru la biashara Afrika.

“Zipo bidhaa nyingi tunazotakiwa kupeleka, tunachohitaji ni kukaa pamoja kuainisha wapi tuanze TCCIA pamoja na wizara wamefanya vizuri kupata vyeti vyote vinavyohitajika kuingia kwenye eneo hilo hatuna kikwazo chochote, twendeni tukafanye biashara kwenye eneo huru la biashara Afrika,” alisema na kuongeza:

“Mwaka jana hatukuingiza bidhaa hata moja kwenye eneo huru la biashara Afrika. Tupo wazalishaji, tupo watoaji huduma, lazima tuongee kwa pamoja na tutoke na maazimio, la lazima yawe maazimio ya kupimika kwamba tarehe moja Julai mwaka 2023 kwamba Watanzania tunapeleka bidhaa 10,” alisema Dk Kijaji.

Alisema ni muhimu Tanzania itumie fursa ya soko la watu bilioni 1.4 kwenye bara hili lenye pato la dola za Marekani trilioni 3.4 hasa ikizingatiwa kuwa nchi hii ni moja ya nchi nane zilizochaguliwa kuanza kunufaika AfCFTA na hakuna kikwazo chochote.

“Mtanzania mfanyabiashara, Mtanzania mwekezaji kupitia faida hizi na fursa hizi huzuiwi kumtafuta agrigator kutoka nchi yoyote Afrika tukaungana kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya soko la Ulaya tukapeleka kuuza huko Ulaya. Hatuzuiwi kuungana ili tufikie viwango vile ambavyo tunajiona sisi kama Tanzania hatuna ili tufikie soko la Marekani.”

Kwa mujibu wa Dk Kijaji, malengo makuu ya AfCFTA ni kuwa na soko moja la bidhaa na huduma hali iliyowaleta pamoja wazalishaji na watoa huduma kama vile CTI na wasafirishaji ambao kwa pamoja wanaangalia aina ya huduma wanazopeleka katika soko huru la biashara Afrika.

Alisema lengo lingine ni kujenga uhuru wa kusafiri kwa wafanyabiashara na mitaji ndani ya Bara la Afrika bila vikwazo vyovyote kwa kusafirisha mitaji kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji miongoni mwa nchi za Kiafrika.

Dk Kijaji alisema faida kubwa ambayo Tanzania inaweza kupata AfCFTA ni kujenga na kukuza uwezo wa uchumi wa viwanda na uzalishaji kupitia uzalishaji wa bidhaa za kilimo na kulisha Afrika nzima.

Mwakilishi wa Sekta Binafsi, Leodgar Tenga alisema Tanzania kujiunga na eneo huru la biashara Afrika ni uamuzi wa kitaifa na alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kulifanya taifa kuwa sehemu ya biashara kimataifa.

Tenga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), alisema wajibu wa sekta binafsi ni kutoa elimu kwa wanachama wake kuhusu nini wafanye ili wabaini na watumie na kufaidika na fursa AfCFTA

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x