Tanzania, Uganda kushirikiana kudhibiti Ebola

TANZANIA na Uganda, zimeingia makubaliano ya kufanya kazi kwa ushirikiano mipakani, ili kudhibiti ugonjwa wa Ebola.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana katika mpaka wa Bugango ulipo Wilaya ya Misenyi, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Issessanda Kaniki.

Pande zote mbili zilikubaliana kushirikiana katika  mambo matatu  ambayo ni kufanya  ukaguzi wa kina kwà wasafiri na kuwapima maambukizi ya ugonjwa wa Ebola na  kutoa cheti, kuweka vifaa vya kuzuia maambukizi, ikiwa ni vitakasa mikono, sabuni na maji tiririka pamoja na kuchukua hatua za pamoja kutoa huduma na kutatua matatizo yoyote yatakayojitokeza.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Issessanda Kaniki, amesema makubaliano waliyoweka ni ya ujirani mwema, ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

“Mkakati huu wa pamoja utasaidia kudhibiti mlipuko wa Ebola kuingia nchini na ikitokea kuna mgonjwa, basi sekta zetu za afya zitashirikiana kwa karibu,”amesema.

Naye ofisa kutoka Mbale, Mlekateka Jesca, amesema Uganda ina ujirani mwema na Tanzania, hakuna shida yoyote tangu Ebola imeingia, kwa upande wao wa Uganda hakuna raia anayevuka kwenda Tanzania bila kuchukua tahadahari, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji yaliyowekwa jiki.

“Sisi kwetu kwa Uganda hatuna shida, bado hatujapata mgonjwa hapa Mbale, ila tunaelimisha wananchi wetu kama hakuna ulazima wa kwenda Mubende na Wilaya zingine zilizoathirika na Ebola basi wasiende,” amesema.

Katika kkao hicho kiliwakilishwa na  wataalamu wa afya kutoka Kituo cha Mbale kwa upande wa Uganda na viongozi mbalimbali wa kata na vijiji, wakati kwa upande wa  Tanzania mbali na Mganga Mkuu wa Mkoa pia walihudhuria viongozi wa Kata ya Bugango.

Habari Zifananazo

Back to top button