TANZANIA na Uganda ndizo nchi pekee za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizofanikiwa kukidhi vigezo vitatu kati ya vinne vilivyoainishwa katika Itifaki ya Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki.
Aidha, Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Mipango limehuisha mpango kazi wa kufikia sarafu moja na kuongeza muda wa utekelezaji wake kutoka mwaka 2024 hadi 2031.
Novemba 2022, wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Masuala ya Uchumi uliofanyika jijini Arusha. Mkutano huo pamoja na mambo mengine, ulijadili tathmini ya utekelezaji wa Mpangokazi wa Miaka Kumi (2014- 2024) wa kufikia sarafu moja ya EAC.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema kwa mujibu wa Ibara ya 5 (3) ya Itifaki ya Umoja wa Fedha, nchi wanachama zilitakiwa kufikia vigezo vya uchumi mpana mwaka 2021 na kuvidumisha kwa muda wa miaka mitatu mfululizo kabla ya kuingia kwenye sarafu moja mwaka 2024.
Alisema vigezo hivyo ni kiwango cha juu cha mfumuko wa bei kisichozidi asilimia 8; kiwango cha juu cha deni la taifa kisichozidi asilimia 50 ya pato la taifa; akiba ya fedha za kigeni ya kutosheleza mahitaji ya miezi minne na nusu; na kiwango cha juu cha nakisi ya bajeti, ikijumuisha misaada kisichozidi asilimia 3 ya pato la taifa.
“Tathmini hiyo imebainisha kuwa, nchi wanachama wa EAC hazijakidhi baadhi ya vigezo vilivyoainishwa katika Itifaki ya Umoja wa Fedha. Aidha, Tanzania na Uganda ndizo nchi pekee zilizofanikiwa kukidhi vigezo vitatu kati ya vinne,” alisema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni.
Kwa mujibu wa Tax, hakuna nchi mwanachama iliyokidhi kigezo cha nakisi ya bajeti, ikijumuisha misaada kutozidi asilimia 3 ya pato la taifa na kuwa kutokana na matokeo ya tathmini hiyo, Mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Mipango ulihuisha Mpango Kazi wa kufikia sarafu moja na kuongeza muda wa utekelezaji wake kutoka mwaka 2024 hadi 2031.
Mpango kazi uliohuishwa umeainisha shughuli zitakazotekelezwa kuwa ni pamoja na kuanzisha taasisi zitakazosimamia utekelezaji wa umoja wa fedha na uoanishaji wa sera za kodi, sera za fedha na sera za viwango vya kubadilisha fedha za kigeni.
Kuhusu mwaka wa fedha uliopita, Bunge la Afrika Mashariki (EALA) lilipitisha miswada miwili ya sheria ambayo ni Muswada wa Sheria ya Kamisheni ya Huduma za Fedha wa EAC wa Mwaka 2022 na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha wa EAC wa Mwaka 2022.
“Kutungwa kwa sheria hizo kunatoa nafasi ya kuanzishwa kwa Kamisheni ya Huduma za Fedha ya Afrika Mashariki kama taasisi ya jumuiya yenye majukumu ya kusimamia utekelezaji wa sera, sheria na taratibu za jumuiya katika sekta ya fedha. Uanzishwaji wa taasisi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ibara ya 21 ya Itifaki ya Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki.