Tanzania, Ujerumani zajadili urejeshwaji mikusanyo

anzania, Ujerumani zajadili urejeshwaji mikusanyo

WATAALAM  na watafiti  wa masuala ya makumbusho na malikale wa Tanzania wakishirikiana na Serikali ya Ujerumani wamekutana  kujadili juu urejeshwaji wa mikusanyo iliyochukuliwa na wakoloni nchini.

Mkutano huo  umefanyika Dar es salaam ukiandaliwa na Taasisi ya Makumbusho ya Taifa kwa ushirikiano na Chuo  Kikuu cha GÖTTINGEN cha Ujerumaini.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dk  Hassan Abbassi, Mhifadhi  Mkuu wa Mambo ya Kale katika Idara ya Mambo ya Kale kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita amesema zaidi ya mikusanyo ya masalia ya malikale 13,550  ipo katika Makumbusho mbalimbali duniani ikiwemo nchini Ujerumani.

Advertisement

Amesema mikusanyo hiyo ikiwemo mabaki ya binadamu ilichukuliwa na wakoloni na  miongoni mwao inahitajika kurudishwa nchini, ili kutumika kwa manufaa  ya kuongeza kipato.

Amesema yapo mataifa makubwa ambayo yameonesha nia ya kurejesha mikusanyo hiyo, hivyo kuna haja ya kuweka utaratibu mzuri wa urejeshwaji.

“Mikusanyo hiyo ikiwa ni pamoja na mabaki ya binadamu, zana za mawe, mabaki ya mimea na wanyama waliotoweka iliyochukuliwa kabla na baada ya ukoloni inabidi irejeshwe nchini kwa utaratibu maalum kwa lengo la kuendelea kuimarisha uhifadhi wa historia na utamaduni wa Taifa la Tanzania,” amesema.

Amesema  Taasisi ya Makumbusho chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Chuo hicho  cha Ujerumani ambao wana mikusanyo mingi wamewakutanisha wadau mbalimbali hata ambao  katika nchi zao masalia kama hayo yalisharudishwa, ili kupata uelewa wa namna ya kuweza kurejesha.

Amesema katika mikusanyo hiyo ipo ambayo huenda isirudi akitolea mfano wa mjusi wa Kitendaguro kutokana na namna alivyounganishwa, jambo linaloweza kuwa ni gharama nchini lakini pia  mingine inaweza kurejeshwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho, Dk Noel Lwoga amesema dunia haswa bara la Afrika na Ulaya wako katika mazungumzo  ya urejeshaji wa masalia hayo yaliyochukuliwa enzi za ukoloni.

“Masalia hayo yalipelekwa nje ya nchi tumenza mikutano ya kujenga uelewa wa pamoja na wadau kutoka vyuo vikuu, jamii, serikalini watafiti na wataalam kutoka Ujerumani  ili kujadili juu ya masalia ya kale hasa ya binadamu na mengineyo  ambayo yalichukuliwa Tanzania wakati wa ukoloni,” amesema.

 

Balozi wa Ujerumani nchini, Dk Regine Hess amesema wao wako tayari kutoa ushirikiano katika urejeshaji, na kusisitiza kuwa ifahamike ilikotoka na namna ya kuihifadhi.

Amesema  Serikali ya  Ujerumani inatamani kuona wakazi wa maeneo ambako mabaki ya malikale yalichukuliwa wanakua na mtazamo chanya kuhusu mambo yaliyofanyika wakati wa ukoloni na kusisitiza watu wamapaswa  kutazama siku za usoni, badala ya kujikita kutazama yaliyopita.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *