TANZANIA na Ujerumani zimekubaliana kuhakikisha wanakuza kiwango cha biashara na uwekezaji kilichopo baina ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na na Rais wa Ujerumani, Frank Steinmeie walipozungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam leo.
Rais Samia alisema ujio wa Rais Steinmeier umezifanya nchi hizo kuingia hatua nyingine ya ushirikiano wa kihistoria uliodumu kwa miaka 60 mpaka sasa.
Alisema katika kipindi hicho chote, Ujerumani imekuwa mdau muhimu wa biashara na uwekezaji wa Tanzania kwa kuwa Ujerumani imewekeza nchini miradi takribani 180 na walikubaliana pia kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Katika hilo, alisema walipanga kuwa na kongamano la biashara na uwekezaji jana kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na wafanyabiashara wa Ujerumani.
“Nimemuhakikishia Rais Steinmeier kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo yajayo ya ushirikiano wa maendeleo yatakayofanyika mwakani,”alisema Rais Samia
Aliongeza”Ziara hii ya Rais Steinmeier inathibitisha dhamira ya serikali zetu mbili katika kukuza na kuimarisha uhusiano nchi zetu na watu wake.”