Tanzania ya 5 kwa wagonjwa wa Selimundu duniani

Wengi wanavinasaba hawajijui

TANZANIA imetajwa kuwa nchi ya tano duniani kwa wagonjwa wengi wa Selimundu huku mikoa ya Pwani na Kanda ya Ziwa ikiongoza kwa wagonjwa

Hayo yamesemwa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa leo Septemba 4,2023 katika uzinduzi wa programu ya ukusanyaji damu salama kwa ajili ya wagonjwa wa Selimundu inayoenda sambamba na utambuzi wa watoto wachanga wenye ugonjwa huo.

Programu hiyo inayoongozwa na Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi (MUHAS) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania.

Lengo ni kukusanya chupa 500 za damu ili kusaidia wagonjwa wa Selimundu.

Profesa Kamuhabwa amesema, Tanzania ni nchi ya nne kwa wagonjwa wa Selimundu Afrika na ya tano duniani ikiongozwa na India, Angola, Congo na Nigeria.

Amesema, mikoa ya Pwani na Kanda ya Ziwa ina idadi kubwa ya watoto wenye Selimundu na hiyo inatokana na mikoa hiyo kuwa na kiwango kikubwa cha ugonjwa wa malaria.

Prof. Kamuhabwa amesema takwimu hizo zimetokana na utafiti uliofanyika katika hospitali ya Muhimbili ambapo pia, watoto 11,000 wanazaliwa kila mwaka wakiwa na tatizo la Selimundu.

Amesema, kutokana na hali hiyo wameanzisha programu maalum katika Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwa asilimia 35 ya wagonjwa wa moyo wana vinasaba vya Selimundu na hivyo kuhitaji matibabu ya juu zaidi.

“Kati ya wagonjwa 100 wa moyo, asilimia 35 wametambulika na kuingizwa kwenye matibabu ya hali ya juu ikiwemo upandikizaji uroto na matibabu ya kijenetiki ‘genes therapy’, ” Amesema.

Akifafanua zaidi, , Makamu Mkurugenzi wa Mtandao wa Wanaopambana na Ugonjwa wa Selimundu Tanzania (Tanscda) ambae pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Elisha Osati amesema takwimu hizo zimetokana na utafiti uliofanywa Muhimbili

Amesema pia kupitia utafiti huo uliofanyika Muhimbili na Bugando Mwanza iligundulika asilimia 15 mpaka 20 ya watanzania wanachembe za Selimundu lakini hawajijui.

“Wenye chembe wengi hawajijui, ubaya unakuja mwanamke ana chembe na mwanaume ana chembe, wanapokutana kimwili na wakazaa mtoto, basi mtoto huyo ndio anazaliwa na ugonjwa wa Selimundu.”Amesema na kuongeza

” Ni vizuri watu wakiwa kwenye mahusiano wasiishie kupima tu ukimwi ila wapime na Selimundu ili waanze matibabu mapema na kuepuka kuzaa watoto wenye Selimundu.” Amesema Dk Osati.

Amesema, vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano, vinachangiwa na ugonjwa wa Selimundu kwa asilimia saba na wakina mama wajawazito wanapata changamoto nyingine za kiafya na wengine kumpoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Nae, Muhadhiri wa MUHAS Prof, kitengo cha Hemotojia Prof. Emmanuel Balandya
amesema ukiacha wagonjwa wa HIV na ajali, Selimundu ni kundi jingine la wagonjwa wanaohitaji damu kwa wingi kitu ambacho kimepelekea kuzinduliwa kwa programu hiyo ya kuchangangia damu kwa wagonjwa wa Selimundu ili watu wachangie zaidi.

“Katavi, Kigoma pia kuna wagonjwa wengi tunachotaka ni serikali kuongeza wigo wa hospital ili waweze kugundulika mapema na kuanzishwa matibabu.

“Kwa sasa tuna wagonjwa zaidi ya 7,000 katika Mikoa minne ya Pwani, Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.” Amesema na kuongeza

” Kwa Tanzania nzima tunakadiria kuwa na wagonjwa 200,000 mpaka 300,000 safari ambayo ni ndefu, faraja ni kwamba tumeshaanza.

Amesema mradi huo wa uchangiaji damu unalenga pia kuwatambua watoto wachanga wanazaliwa.

“Vituo vyetu vya majaribio ni Amana na Bugando matokeo ambayo tumeyaona yametupa faraja tukipata vifaa tunaweza kutoa matibabu ya uhakika, tumeshawasiliana na Wizara na Waziri Ummy Mwalimu anatoa sapoti kubwa majadiliano yanaenda.” Amesema Prof. balandya

Amesema, mwongozo umeshatengenezwa na hivi sasa zoezi la kuusambaza katika hospitali zote za Mikoa na Wilaya kinaendelea ili wajue namna bora ya kuhudumia wagonjwa wa Selimundu.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button