Tanzania ya pili Afrika kwa usalama wa taarifa binafsi
DAR ES SALAAM: TANZANIA ni ya pili kwa usalama wa ulinzi wa taarifa binafsi mtandaoni kwa Bara la Afrika.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ameeleza hayo leo Aprili 3, 2024 akinukuu taarifa ya Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano la (ITU) kwa kusaidiana na Shirika la Kimataifa Kimataifa linaloshughulikia Usalama Mtandaoni ‘the Global Cybersecurity Index’ kwenye uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema, uwepo wa sheria tatu muhimu zinazosimamia usalama mtandaoni, yaani; Sheria za Makosa ya Mtandao 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki 2015 na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa binafsi ya mwaka 2022 na uwepo wa taasisi imara kama TCRA na sasa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni moja ya vigezo vinavyofanya Tanzania kuwa ya pili kwa usalama Mtandaoni katika bara la Afrika
“Pia, tukio hili la leo linaingiza Tanzania katika horodha ya nchi za wastaarabu duniani,” amesema Nape.
Amesema, takwimu zinaonyesha kuwa nchi mbalimbali zimetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kama ambavyo imebainishwa; Nchi 162 kati ya nchi 198 Duniani zimetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Nchi 36 kati ya nchi 54 za Afrika zimetunga Sheria hiyo; Nchi 12 kati ya nchi 16 za SADC zimetunga Sheria hiyo; Nchi nne kati ya nchi saba za Afrika Mashariki zimetunga Sheria hiyo.
Amesema kwa Afrika Mashariki nchi ambazo bado hazijatunga sheria hiyo ni Burundi, Sudani ya Kusini na Somalia.