Tanzania yahimiza ushirikiano zaidi majeshi Afrika Mashariki

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda ametaka vikundi vya ulinzi na usalama vinavyoshiriki zoezi la Ushirikiano Imara 2023 kwa majeshi ya nchi za Afrika ya Mashariki kuhakikisha vinaliwakilisha vema taifa ili kujenga ushirikiano zaidi na nchi jirani.

Akizungumza baada ya ufunguzi uliofanyika mjini Musanze, Rwanda, Jenerali Mkunda alitaka zoezi hilo kuwa chachu ya kujifunza namna ya kutatua changamoto za kiulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwa wananchi wanategemea majeshi yao kupata msaada wa ulinzi na uokozi majanga yanapotokea.

Katika ufunguzi huo uliofanyika Jumapili, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Juvenal Marizamunda alikabidhi bendera ya kuashiria kuanza ambapo mkuu wa zoezi hilo, Dk Alice Urusaro Uwagaga Karekezi aliyekabidhi bendera hiyo kwa Mkuu wa Majeshi ya Kikanda (REMIKA), Brigedia Jenerali Julius Gambosi.

“Unajua hakuna kitu kikubwa kinachojenga imani ya wananchi kwa majeshi yao kama kupewa msaada wa kijamii pindi wapatapo majanga. Imani yao kubwa hubaki kwa wanajeshi ambao ndio huwa wa kwanza kutoa msaada,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkunda, vikundi vinavyoshiriki vinapaswa kudumisha udugu na ushirikiano baina yao na majeshi mengine kutoka nchi za EAC.

“Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikisifika kwa kuwa rafiki wa kweli katika nchi za EAC, Afrika na dunia kwa ujumla hivyo, hakikisheni mnaendelea kuwa mfano bora wa kuigwa,” alisema. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa na kuongeza kuwa ni wakati sahihi kufanya kazi pamoja kwa kuwa majanga yanapotokea, mamlaka huhusika kwa njia mbalimbali ikiwamo ya utoaji wa elimu na utaalamu kuhusu namna ya kukabiliana na majanga.

“Tupo tayari kufanyakazi na majeshi ya ulinzi na usalama kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu ya kihabari na kusaidia kufanikisha majukumu ya kulinda amani ili kurudisha imani ya wananchi majanga yanapotokea,” alisema.

Zoezi linalenga kuvijengea vikundi vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za kiraia uwezo wa kukabiliana na ugaidi, uharamia, menejimenti ya majanga pamoja na ulinzi wa amani katika ukanda wa EAC. Wengine miongoni mwa walioshiriki, walitoka katika majeshi yakiwamo Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Kituo cha Taifa cha Kukabiliana na Mapambano dhidi ya Ugaidi. Aidha, Taasisi za kiraia zilizoshirikishwa ni pamoja na zilizo chini ya sekta za habari, haki za binadamu, usawa wa kijinsia, diplomasia na ushirikiano wa kimataifa kutoka nchi za EAC.

Habari Zifananazo

Back to top button