Tanzania yaichapa Ufaransa kombe la Dunia

Balozi wa Tanzania nchini India ataka mshikamano kuikabili Canada

LICHA ya kucheza pungufu dakika za lala salama, timu ya soka ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17, Serengeti Girls,  imeichapa Ufaransa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali za Kombe la Dunia inayoendelea India.

Mabao ya wasichana hao shupavu wa Kitanzania yamefungwa na Diana Mnally dakika ya 16 huku Christer Bahera akiweka kimiani la pili kwa mkwaju wa penalti dakika 56.

Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Fatorda uliopo mji wa Goa, Serengeti Girls ilitawala kipindi cha kwanza lakini Ufaransa ilizinduka kipindi cha pili na kupata bao kwa mkwaju wa penalti kupitia Lucie Calba dakika 75.

Katika mchezo wa kwanza Tanzania iliyopo kundi D ilipoteza dhidi ya Japan kwa mabao 4-0.

Tanzania itacheza mechi ya mwisho ya makundi Oktoba 18 dhidi ya Canada.

Balozi wa Tanzania nchini India, Anisa Mbega akiwa na wachezaji wa Serengeti Girls

Akizungumza na HabariLeo baada ya mechi kumalizika, Balozi wa Tanzania nchini India, Anisa Mbega amekipongeza kikosi hicho huku akiwataka Watanzania kuomba zaidi kuelekea mchezo unaofuata dhidi ya Canada.

“Nawapongeza sana Timu yetu Serengeti Girls U-17 kwa ushindi huu! Naamini na mechi ijayo tutafanya vizuri zaidi. Dua na sala zetu bado zinahitajika ili kuweza kuifunga Canada na kwenda hatua zitakazofuata,” Mwanadiplomasia huyo ameeleza. 

Wakati huo huo Timu ya soka ya taifa ya wavulana chini ya miaka 17(Serengeti Boys) imeshika nafasi ya tatu katika michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Kanda wa CECAFA inayoendelea Ethiopia baada ya kuifunga Uganda kwa penelti 4-1.

Habari Zifananazo

Back to top button