Tanzania yaieleza dunia inavyothamini maji

WIZARA ya Maji imesema Rais Samia Suluhu Hassan anaipa umuhimu ajenda ya upatikanaji maji safi na salama kwa kutambua kuwa utachangia kumuinua mtoto wa kike na mwanamke ili waweze kutumia muda zaidi katika elimu na shughuli za kiuchumi.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema hayo wakati wa mjadala wa Uongozi na Usimamizi wa Masuala ya Maji ambao uliandaliwa na nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania na Afrika Kusini.

Mjadala huo pia ulishirikisha mashirika ya kimataifa anuai yakiwamo ya GWP, UNICEF na UNDP na kuhudhuriwa na Dk Jakaya Mrisho Kikwete, Rais mstafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa GWPSA na Mwenyekiti Mwenza wa Jopo la Viongozi Maarufu kuhusu Uwekezaji katika Sekta ya Maji.

Aweso alisema uongozi wa Rais Samia upo makini katika agenda hiyo kwa kuongeza msukomo na utashi wa kisiasa, kuongeza bajeti ya maji na kumarisha taasisi zinazohusiana na usimamizi wa huduma za maji na utekelezaji wa miradi ya maji.

Awali Aweso alimwakilisha Rais Samia katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu maji uliofanyika Umoja wa Mataifa, New York nchini Marekani.

Aweso alihutubia mkutano huo na akabainisha umuhimu wa dunia kukaa pamoja na kusimamia ajenda ya maji, thamani ya maji katika maisha na uchumi, kuongeza uwekezaji katika eneo la maji, ushirikiano wa kimataifa katika maji na utafutaji wa fedha kwa ajili ya maji.

Katika mkutano Tanzania ilibeba ajenda mbili ambazo ni utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Tatu (Water Sector Development Programe III) ambayo inahitaji Dola za Marekani bilioni 6.47 katika kipindi cha 2022-2025.

Vile vile, Tanzania ilikuwa na ajenda ya uwekezaji katika Sekta ya Maji ili kufikia Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Tanzania Water Investment Programme 2023-2030).

Programu hiyo inayotarajiwa kuzinduliwa Mei mwaka huu inakadiriwa kuwa na bajeti ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 25.

Habari Zifananazo

Back to top button