Tanzania yaingia 10 bora mapato ya utalii

DODOMA; SERIKALI imesema ongezeko la watalii limeiwezesha Tanzania kwa mwaka 2023 kuingia katika nchi 10 bora zenye mapato zaidi yatokanayo na shughuli za utalii ikiwa ni nchi ya 3 Afrika baada ya Morocco na Mauritius.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Mei 31, 2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

“Aidha, Tanzania imekuwa Nchi ya 9 duniani ikitanguliwa na Serbia, Pakistan, Uturuki, Romania, Ureno, Mauritius, Morocco na Latvia ambazo mapato yake ya Sekta ya Utalii yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 28 ikilinganishwa na rekodi za mwaka 2019 kabla ya janga la UVIKO-19,” amesema Waziri Kairuki na kuongeza:

“Katika hatua nyingine, Tanzania imefanikiwa kurekodi idadi ya juu zaidi ya watalii wa kimataifa iliyofikia asilimia 53 katika kipindi cha Januari hadi Machi 2024 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2019 kabla ya UVIKO-19.

“Ongezeko hilo limeitambua Tanzania kama nchi ya 5 duniani ikitanguliwa na Qatar, Albania, Saudi Arabia na El Salvador na ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watalii.

“Aidha, kwa upande wa mapato yatokanayo na utalii, Tanzania imeendelea kufanya vyema na kushika nafasi ya 4 duniani ikitanguliwa na Serbia, Uturuki na Pakistan kwa ongezeko la asilimia 62 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha robo ya kwanza kabla ya UVIKO-19 Mwaka 2019.

“Taarifa hizi ni kwa mujibu wa World Tourism Barometer ya Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Mei, 2024,” amesema Waziri Kairuki.

Habari Zifananazo

Back to top button