Tanzania yaiomba Indonesia ushirikiano mifumo ya kodi

DODOMA: SERIKALI imeiomba Indonesia ishirikiane na Tanzania kuboresha mifumo ya kodi. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alitoa ombi hilo Dodoma alipokutana na kuzungumza na Balozi wa Indonesia nchini, Tri Yogo Jatmiko.

Dk Mwigulu amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto ya idadi ndogo ya walipa kodi na kuwa kuna wafanyabiashara wengi katika sekta isiyo rasmi hivyo unahitajika mfumo wa kodi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuongeza idadi ya walipa kodi.

SOMA: ‘Uhusiano Tanzania, Indonesia utandelea kudumu’

Amesema Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa ya mifumo ya kodi na kwamba Tanzania itanufaika na ujuzi huo kwa kuwapa ujuzi zaidi maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha kwa ujumla kujifunza katika eneo hilo.

Dk Mwigulu ameishukuru Indonesia kwa mchango wake katika maendeleo ya nchi. Alisema nchi hiyo imesaidia miradi ya kiuchumi na kijamii na imetoa ujuzi na utaalamu kwa Watanzania katika nyanja mbalimbali.

Naye Balozi Tatmiko amesema nchi hiyo iko tayari kuendelea kuwapa ujuzi Watanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta za nishati, kilimo na biashara.

Amesema pia nchi hiyo iko tayari kuwajengea uwezo watumishi wa TRA kuhusu namna ya kujenga na kutumia mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato.

Juni 22, 2023 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefungua rasmi ubalozi wake jijini Jakarta nchini Indonesia.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ubalozi huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, amesema kufunguliwa kwa ubalozi huo kutaziwezesha Serikali ya Tanzania na Serikali ya Indonesia kukuza na kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na kukuza uchumi.

“Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Indonesia hivyo tunaamini kuwa kufunguliwa rasmi kwa ubalozi wetu jijini hapa kutaongeza ushirikiano zaidi baina ya mataifa yetu mawili hususan katika sekta ya uchumi,” amesema Dk Tax.

Waziri Tax ameongeza kuwa Indonesia imefika mbali kiuchumi, hivyo ushirikiano wake na Tanzania utatoa fursa kwa Tanzania kupiga hatua na kuhakikisha bidhaa za mazao ya kilimo na madini zinaongezwa thamani na kuuzwa katika masoko mbalimbali ya kimataifa na kuiwezesha Tanzania kukuza uchumi wake.

Habari Zifananazo

Back to top button