WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekaribisha watu kutoka mataifa mbalimbali kuja Tanzania kwa kuwa ina wananchi wakarimu, wapenda amani, utulivu na ina vivutio vya utalii vinavyotambulika na kukubalika duniani.
Majaliwa alisema hayo jana jijini Arusha wakati anafungua Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheni ya Afrika. Alifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema Tanzania imebarikiwa vivutio vya asili na visivyo vya asili ukiwamo Mlima Kilimanjaro ambao ndio mrefu zaidi Afrika unaoweza kuonekana popote kwa kutumia vyombo vya kielektroniki, lakini ili mtu aupande lazima aje Tanzania.
Aidha, alisema kuna Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayosifika kuwa na idadi kubwa ya wanyama aina ya nyumbu wanaohama, Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro inayojulikana kama Bustani ya Eden ya Afrika na visiwa vya marashi ya karafuu Zanzibar vyenye fukwe za kuvutia zilizopo pwani ya mwambao wa Bahari ya Hindi.
“Na Tanzania ina watu wakarimu wenye makabila zaidi ya 120 wenye mila na tamaduni mbalimbali, lakini wote wanaunganishwa na Lugha ya Kiswahili,” alisema Majaliwa.
Alisema nchi hiyo ina vivutio zaidi vya wanyama kama vile mbuga ya Tarangire iliyopo jirani na Jiji la Arusha, Ziwa Manyara lenye ndege wengi wa kila aina, mbuga ya Katavi yenye twiga weupe pekee duniani na mbuga za Selous, Mikumi, Ruaha na Hifadhi ya Taifa Gombe anakopatikana mnyama aina ya sokwe.
Waziri Mkuu alieleza kuwa kuna maeneo binafsi ya kufugia wanyamapori ambako watalii wana uwezo wa kuchezea hadi sharubu za simba bila kujeruhiwa yaliyopo Arusha na Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Alisema Hifadhi ya Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro ni maeneo yaliyowekwa kwenye orodha ya maajabu saba ya asili ya Afrika na majarida ya New York Times yameitaja Tanzania kama kivutio bora cha kutembelea Afrika na mtandao wa Fox News uliitaja Ngorongoro kuwa ni moja ya mabonde yanayovutia zaidi duniani.
“Na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilipokea tuzo ya hifadhi bora Afrika mara tatu mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 kupitia tuzo za World Travel Awards,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema utajiri huo wa Tanzania katika sekta ya utalii, umeifanya sekta hiyo kuwa mhimili muhimu katika uchumi wa nchi hiyo.
Alieleza kuwa mwaka 2019 kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, mapato yaliyotokana na sekta ya utalii yalifikia dola za Marekani bilioni 2.6 na kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja milioni 1.5 na katika kipindi hicho sekta ya utalii ilichangia wastani wa asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) na asilimia 25 ya mauzo.
Hata hivyo, alisema kama ilivyotokea sehemu nyingine duniani, sekta ya utalii nchini ni kati ya sekta zilizoathirika zaidi na janga la Covid-19.
Hali hiyo ilisababisha idadi ya watalii wa kimataifa kupungua kwa asilimia 59 kutoka watalii milioni 1.5 mwaka 2019 hadi kufikia watalii 620,867 mwaka 2020.
Alifafanua kuwa kutokana na janga hilo, mapato yaliyotokana na sekta hiyo yalipungua pia kutoka dola za Marekani bilioni 2.6 hadi kufikia dola za Marekani milioni 714.59 sawa na upungufu wa asilimia 72.5.
Majaliwa alisema kwa kutambua umuhimu wa utalii nchini, serikali ilichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na Covid-19 ili kuinusuru sekta hiyo ambazo zimezaa matunda na sekta hiyo imeanza kurejea kama ilivyokuwa awali kabla ya ugonjwa huo.
Alisema takwimu za mwaka 2021 zinaonesha watalii wameongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 922,992 mwaka 2021 na mapato yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka dola za Marekani 714.59 mwaka 2020 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021.
Alisema takwimu za mwaka huu zinaonesha sekta ya utali inazidi kuimarika hasa baada ya uzinduzi wa filamu iliyomshirikisha Rais Samia ya ‘Tanzania: The Royal Tour.’ Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya mwongozo uliotolewa na UNWTO kwa nchi wanachama ikiwamo Tanzania katika kukabiliana na athari za Covid-19. Kuhusu mkutano huo wa 65 wa Kamisheni ya Afrika, alisema amejulishwa kuwa utakuwa na jukwaa la masoko litakalotoa fursa kwa wataalamu nguli wa masuala ya masoko katika sekta ya utalii kuwasilisha mada zitakazowajengea uwezo wadau wa sekta ya utalii nchini.
Alimpongeza Katibu Mkuu Mtendaji wa UNWTO, Zurab Pololikashvili na washiriki wa mkutano huo, kuungana na Tanzania katika jitihada za kutunza mazingira kwa kupanda miti baada ya mkutano na kuagiza miti hiyo itunzwe ili dhamira ya kupandwa kwake itimie.
Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana alisema mkutano huo umehudhuriwa na washiriki na mawaziri kutoka zaidi ya nchi 33 wanachama wa UNWTO.
Alisema mkutano huo utawajengea uwezo wadau wa sekta ya utalii katika kutangaza utalii, kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii kuendana na malengo ya nchi ya kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025 na mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa kufikia dola za Marekani bilioni sita.
Pololikashvili aliipongeza Tanzania kupiga hatua ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini licha ya janga la Covid-19 kutokea ikiwamo filamu ya ‘Tanzania: Royal Tour’ iliyowezesha watalii kutoka nje kutembelea nchi kwa utalii na kuangalia fursa za uwekezaji.
Imeandikwa na Halima Mlacha (Dar) na Veronica Mheta (Arusha).