Tanzania yajipanga kufanikisha jukwaa la kimataifa AGRF-2023

IKIWA na lengo la kuwa kitovu cha uhakika wa chakula kimataifa, Tanzania inayosifika kwa uzalishaji wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki imeanza kujiandaa kwa nguvu na kasi kubwa Mkutano wa AGRF-2023 (Jukwaa la Mifumo ya Chakula ya Afrika 2023) unaotarajiwa kufanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 4 hadi 8, 2023.

Ikiwa sehemu ya maandalizi ya mkutano huo unaotarajiwa kuwa na wageni 3,000 matukio matatu muhimu yamefanywa na watendaji wa serikali ikiwamo uzinduzi wa Tanzania Agribusiness Deal Room, ambayo husaidia ushirikiano na uwekezaji katika mlolongo wa thamani ya mifumo ya chakula, Mkutano wa Value4Her Women in Agribusiness, unaowawezesha wanawake wajasiriamali na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu na kuanzisha mchakato wa usajili kwa ajili ya Mkutano wa AGRF-2023.

Matukio yote hayo yamefanyika kama sehemu ya kuonesha fursa na yameelezwa na wataalamu na wadau mbalimbali wa kilimo kuwa ni kuonesha dhamira ya Tanzania ya kuwavutia wawekezaji na kuendesha mabadiliko ya kimkakati katika sekta ya kilimo.

Mkutano huo mtarajiwa ambao umendaliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Kundi la Wadau wa AGRF umelenga kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo. Tanzania katika mkutano huo umelenga kuonesha mafanikio yake, kuonyesha uwezo wake mkubwa, na kuwavutia wawekezaji wa ndani na kimataifa wanaotafuta miradi ya kilimo yenye matumaini.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, anasema Mkutano huo unatarajiwa kuwaleta pamoja viongozi zaidi ya 3,000 kutoka bara la Afrika kujadili mabadiliko ya mifumo ya chakula na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa wote.

Anasema chini ya uongozi wa maono wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha uwekezaji cha kipekee barani Afrika.

Wakati Bashe, akizindua mchakato wa usajili kwa Mkutano wa AGRF-2023 Mei 12,2023 huko Dodoma kwa  kuwaalika wadau wa kilimo duniani kujisajili na kushiriki katika tukio hilo muhimu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, yeye alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula ya Afrika (AGRF), Amath Pathé Sene  na  kujadiliana naye jinsi mkutano wa kilimo wa AGRF unavyoweza kuhamasisha fursa za uwekezaji katika sekta ya mifugo na uvuvi nchini Tanzania.

“Katika mkutano wa AGRF, washiriki watakuwa na fursa muhimu ya kuona mafanikio na shughuli za wakulima wa Tanzania, wakipata ufahamu muhimu juu ya mazoea mazuri ndani ya sekta ya kilimo,” alibainisha Sene.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ,Profesa Riziki Shemdoe, Mei 11, 2023,  akizundua rasmi Tanzania Agribusiness Deal Room jijini Dar es Salaam alisema:”Agribusiness Deal Room ni nafasi yenye mwingiliano mkubwa kwa wahusika mbalimbali kushiriki na kuendeleza majadiliano katika ushirikiano wa pande mbili na pande nyingi. Hii, kwa upande wake, inasaidia kuongeza uwekezaji katika mlolongo wa thamani wa mifumo ya chakula,” alisema Profesa Shemdoe.

Na Mei 12, Profesa Shemdoe, alizindua rasmi Mkutano wa Value4Her Women in Agribusiness ambapo alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika sehemu ya biashara na kuvutia wawekezaji.

Meneja wa Nchi  wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA) nchini Tanzania,  Vianey Rweyendela alisisitiza umuhimu wa  nchi kuwa kitovu cha uwekezaji katika sekta ya biashara ya kilimo. .

 

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button