Tanzania yang’ara tuzo za utalii Afrika
HIFADHI ya Taifa Serengeti imeshinda tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa mwaka 2022 na kuifanya hifadhi hiyo kuwa hifadhi bora Afrika kwa mara nne mfululizo.
Utoaji wa tuzo hizo zinazoandaliwa na Taasisi ya World Travel Awards (WTA), ulifanyika juzi jijini Nairobi nchini Kenya.
Kwa mujibu wa tovuti ya WTA, Mwanzilishi wa taasisi hiyo, Graham Cooke akizungumza kwenye sherehe hizo za Nairobi, alisema ushindi huo ni kutambua mchango wa taasisi au kampuni zinazotoa huduma bora Afrika.
Kwa ushindi huo wa Hifadhi ya Serengeti imezishinda hifadhi nyingine Afrika zikiwamo Central Kalahari Game Reserve ya Botswana, Etosha National Park ya Namibia, Kidepo Valley National Park ya Uganda, Kluger National Park ya Afrika Kusini na Masai Mara National Reserve ya Kenya.
Rais Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na ushindi huo na amewapongeza wadau wote wanaoshiriki katika uhifadhi nchini.
“Nimefurahishwa na ushindi wa tuzo wa mara ya nne mfululizo wa hifadhi yetu ya taifa ya Serengeti kuwa hifadhi bora barani Afrika. Nawapongeza wadau wote wanaoshiriki katika uhifadhi hapa nchini na nawaomba wananchi tuendelee kuunga mkono uhifadhi ili kukuza uchumi kupitia utalii,” ameandika Rais Samia katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter.
Katika tuzo hizo, Zanzibar imeibuka mshindi wa Tuzo ya Eneo la Fukwe Bora Afrika kwa mwaka 2022 na kuifanya kuwa eneo bora la fukwe Afrika kwa mara ya pili mfululizo. Iliwahi pia kushinda tuzo hiyo mwaka 2013.
Aidha, katika tuzo hizo, Kisiwa cha Thanda kilichopo wilayani Mafia mkoani Pwani kimeshinda Tuzo ya Kisiwa Binafsi cha Kifahari cha Utalii Afrika mwaka 2022, huku Tuzo ya Hoteli Bora ya Kifahari Afrika kwa ajili ya utalii ikienda kwa Hoteli ya Four Seasons Safari Lodge-Serengeti ya Tanzania.
Aidha, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeibuka Bodi Bora ya Utalii Afrika kwa mwaka 2022, ikishinda kwa mara ya kwanza tangu tuzo zilipoanza kutolewa mwaka 2008.
Bandari ya Dar es Salaam imeteuliwa kuwania tuzo za WTA katika Kipengele cha Bandari Bora za Huduma Duniani kwa mwaka 2022, ikishindanishwa na bandari nyingine 19. Upigaji kura umefunguliwa na zitafungwa Oktoba 20, mwaka huu ili kupisha kutangaza washindi.
Aidha, Zanzibar imeteuliwa kuwania tuzo ya dunia ya kisiwa chenye fukwe bora zaidi duniani na katika kinyang’anyiro hicho inashindana na visiwa vingine 18 vilivyoingia kuwania tuzo hiyo.
Pia Tanzania imeingizwa kuwania Tuzo ya Eneo Bora la Utalii Duniani na inachuana na nchi nyingine nane huku pia TTB pamoja na kushinda Tuzo ya Bodi Bora ya Utalii Afrika, imeteuliwa pia kuwania tuzo hiyo duniani mwaka huu na matokeo yatatangazwa mwezi ujao.
Tuzo za WTA zilianzishwa mwaka 1993 ili kutambua, kutunza na kusherehekea ubora katika sekta zote muhimu za huduma zikiwamo usafiri, utalii na ukarimu.
Akizungumza kwenye hafla ya kuwatunza washindi juzi, Cooke alisema WTA inatambua mchango wa watoa huduma hivyo kushinda kwao kunawawezesha kutambulika zaidi.