TANZANIA imechaguliwa miongoni mwa nchi 48, kati ya nchi 193 wanachama wa ITU kuwa katika Baraza la Shirika la Mawasiliano duniani (ITU) kwa mwaka 2023 hadi 2026.
Baraza la ITU ni chombo cha Shirika la Mawasiliano Duniani, chenye mamlaka ya kusimamia masuala ya kisera ya mawasiliano ya simu, ili kuhakikisha kuwa shughuli za ITU, sera na mikakati inasimamiwa kikamilifu kwa kuzingatia mazingira ya mawasiliano yanayobadilika kwa kasi.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameeleza dhamira ya Tanzania katika ITU kwa miaka 4 itakayokuwa katika baraza hilo.
“Napenda kusisitiza kuwa Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi nyingine wanachama, sekretarieti ya ITU na ofisi za Kanda, ili kuifanya ITU kuwa chombo muhimu cha kimataifa, ambacho kina mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zote wanachama kama mjumbe wa Baraza la ITU,” alisema Waziri Nnauye.