Tanzania yang’ara utalii wa tiba EAC
TANZANIA imetajwa kung’ara katika utalii wa tiba kutokana na watu kutoka nchi mbalimbali zikiwamo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujitokeza kwa wingi kupata matibabu ya kibingwa kwa magonjwa tofauti hususani moyo, mifupa na saratani.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema tangu Julai 2022 hadi Machi 2023, wagonjwa 812 kutoka nchi hizo za ukanda, wamehudumiwa nchini katika hospitali za taifa, hospitali maalumu na za kanda.
Julai 2021 hadi Machi 2022, idadi ya waliofika nchini kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini ilikuwa 368, hali inayoonesha kuwapo ongezeko kubwa.
Licha ya nchi za EAC, wengine wametoka nje ya ukanda hususani nchi za Zambia, Comoro, Zambia, Malawi na Msumbiji kwa ajili ya kupata matibabu nchini.
Katika hotuba ya bajeti ya wizara yake aliyoisoma bungeni wiki iliyopita, Ummy alielezea utendaji kazi wa hospitali zinazotoa huduma za kibingwa nchini ikiwamo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema utalii wa tiba umeendelea kuimarika nchini baada ya uamuzi wa serikali kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hali inayozidi kuvutia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali kuzifuata Tanzania.
“Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma hizo na kuanzisha nyingine ili Tanzania iwe kitovu cha utalii tiba barani Afrika,” alisema Ummy.
Kuhusu Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, Ummy alisema ilifanikiwa kutoa huduma za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa 11 na kwamba, huduma hizo ni za kwanza kufanyika katika Afrika Mashariki na Kati.
Alisema wagonjwa 84 kutoka Comoro, Kenya, Uganda, Korea, Canada, Misri na China walipatiwa huduma mbalimbali katika hospitali hiyo.
Akizungumzia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Waziri Ummy alisema huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zilizotolewa na taasisi katika kipindi hicho kuwa ni pamoja na uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo, kufunga vifaa visaidizi vya moyo, kuzibua mishipa ya damu ya moyo na kutibu hitilafu za mfumo wa umeme wa moyo.
“Taasisi pia imefanya upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua na mishipa ya damu kwa wagonjwa 502. Kati ya hao, wagonjwa 397 walikuwa watu wazima na 105 walikuwa watoto. Watu wazima 170 wenye matatizo kwenye mishipa ya damu walifanyiwa upasuaji wa mishipa ya damu,” alisema.
Katika kuthibitisha kuimarika kwa uwezo wa taasisi hiyo, Ummy alisema hospitali hiyo ilifanikiwa kufanya upasuaji mgumu kwa uwezo wa wataalamu katika utoaji huduma kwa magonjwa ya moyo.
Aidha, ilifanya upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo maalumu.
Alisema katika huduma hizo, wagonjwa 1,069 walipatiwa matibabu ya moyo na kati yao, 884 sawa na asilimia 82.6 walikuwa ni watu wazima na 165 sawa na asilimia 17.4 walikuwa watoto.
Katika hatua nyingine, Ummy alisema taasisi imetoa huduma kwa wagonjwa 14 wenye shida ya mfumo wa umeme wa moyo.
Alisema hospitali hiyo ilihudumia wagonjwa 92 kutoka nje ya nchi, ikilinganishwa na wagonjwa 58 waliohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22.
Kwa mujibu wa waziri huyo, wagonjwa hao walitoka Burundi, Comoro, Rwanda, Uganda, Kenya, Cameroon na Zambia.
Katika hotuba yake bungeni, Ummy alizungumzia pia Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kusema Julai 2022 hadi Machi, 2023 ilifanya upasuaji kwa wagonjwa 5,477.
Alisema upasuaji huo ulikuwa wa mifupa, kubadilisha nyonga, upasuaji wa goti, upasuaji wa goti kwa kutumia matundu na upasuaji wa mfupa. Pia MOI inaendelea kutumia mtambo maalumu wa kuchunguza na kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu.
“Taasisi ilipokea wagonjwa 176 ikilinganishwa na wagonjwa 162 waliohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22. Wagonjwa hao walitoka katika nchi za Kenya, Uganda, Congo, Zambia na Comoro,” alisema.
Kuhusu Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Ummy alisema ilitibu wagonjwa kutoka nchi za nje ikiwa ni pamoja na nchi za ukanda wa Afrika.
Alisema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, wagonjwa 176 walihudumiwa ikilinganishwa na wagonjwa 162 katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22. Wagonjwa hao walitoka katika nchi za Kenya, Uganda, Congo, Zambia na Comoro.
Aidha, wagonjwa 152 kutoka nje ya nchi walipatiwa huduma za uchunguzi na tiba ya saratani ikilinganishwa na wagonjwa 148 waliopata huduma hizo katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22. Wagonjwa hao walitoka katika nchi za Malawi, Kenya, Comoro, DRC, Msumbiji, Sudan Kusini, Zambia na Uganda.