Tanzania yaondolewa kwenye orodha ya madeni makubwa
TANZANIA imeanza vizuri mwaka 2024 baada ya kuondolewa kwenye orodha ya nchi zenye madeni makubwa Afrika.
Taarifa ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) jana iliyotoa orodha ya nchi 10 zenye madeni makubwa Afrika, ilisema kitendo hicho cha Tanzania kuondolewa kwenye orodha hiyo kimetokana na kufanya vizuri kiuchumi na usimamizi mzuri wa fedha.
“Inaweza kuwa ishara nzuri na chanya kwa wawekezaji na taasisi za kifedha za kimataifa kwani inaashiria kuwa kiwango cha madeni cha Tanzania kinadhibitika kulinganisha na nchi nyingine katika ukanda wake,” ilisomeka taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema hali ya Tanzania kuondolewa kwenye orodha hiyo itaongeza hali ya kujiamini na kuvutia wawekezaji zaidi jambo ambalo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Mtu anaweza kulinganisha kati ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika kama Kenya, ambayo imekumbwa na msukosuko wa madeni makali na kuifanya kuingia kwenye majadiliano na watoa mikopo na kuomba msaada kwa taasisi za kifedha za kimataifa,” ilisomeka taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kenya ina deni la Dola za Marekani zaidi ya bilioni mbili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ina deni la Dola za Marekani bilioni 1.29, Morocco Dola bilioni 1.499, Nigeria Dola bilioni 1.8.
Misri ina deni la Dola za Marekani bilioni 11.96, Angola bilioni 3.1, Afrika Kusini bilioni 2.66, Ivory Coast bilioni 2.1, Tunisia bilioni 1.2.
Taarifa hiyo ilisema nchi hizo zimekumbwa na madeni makubwa kutokana na kupitia changamoto ya homa ya Covid-19.
Mara kadhaa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwa nchi itakopa kwa kuangalia njia rahisi zitakazofaa.
“Kwa vyovyote vile tutakopa, tutaangalia njia rahisi zitakazotufaa kukopa kwa maana fedha hizi hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani,” alisema Samia akizungumzia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Ikulu Dar es Salaam mwaka 2021.
“Niwaombe ndugu zangu mnaosimamia hii sekta (sekta ya mikopo) twendeni, mimi niko pamoja nanyi tutasimama kuangalia mikopo inayotufaa tukiongozwa na Gavana wa Benki Kuu na Waziri wa Fedha yuko hapa, atatuongoza mikopo gani itatufaa tutachukua tumalize reli hii muda uliopangwa ili iweze kutengeneza fedha tulipe mikopo tunayochukua,” alisema.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, deni la Serikali hadi Aprili 2023, lilikuwa Sh trilioni 79.10, sawa na ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na Sh trilioni 69.44 Aprili 2022.
Sh trilioni 27.94, sawa na asilimia 35.3 na deni la nje ni Sh trilioni 51.16, sawa na asilimia 64.7.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, kati ya deni la nje, deni lenye masharti nafuu ni Sh trilioni 37.69, sawa na asilimia 73.6, hivyo, sehemu kubwa ya deni la nje ni mikopo yenye masharti nafuu.
Tathmini ya uhimilivu wa deni la serikali iliyofanyika Desemba 2022 ilionesha kuwa deni la serikali ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu.
Kwa mujibu wa Mwigulu matokeo ya tathmini yanaonesha uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 32.
5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 18.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40.
Aidha, uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 120 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.
Alisema uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa asilimia 60 mauzo ya bidhaa na huduma nje ni asilimia 13.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 15.
Katika kuhakikisha kuwa deni la serikali linaendelea kuwa himilivu, serikali inatekeleza hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha mikopo inayopewa kipaumbele ni ile yenye masharti nafuu kadri inavyopatikana.
Hali hiyo inajidhihirisha katika bajeti ya 2023/24 ambapo mikopo nafuu imeongezeka kwa asilimia 22.8 na yenye masharti ya kibiashara imepungua kwa asilimia 14.4.