Tanzania yapaa kimataifa vita dhidi ya rushwa

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamdun amesema Tanzania imetambulika kuwa ni moja ya nchi chache Afrika zilizopiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa.

Alibainisha kuwa hatua hiyo imetokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika kuhusu hali ya rushwa duniani ambapo Tanzania imepanda katika eneo hilo la udhibiti wa vitendo vya rushwa.

Aidha, alisema juhudi za serikali kuimarisha mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika kufanikisha malipo na utoaji wa baadhi ya huduma, zimeleta mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa.

Akizungumza wakati wa mkutano wa mwaka wa viongozi wa taasisi hiyo uliomalizika juzi Dodoma, alisema mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa yanabainishwa pia katika vipimo vya kimataifa kuwa Tanzania inapiga hatua.

Pia, alisema matokeo ya utafiti wa kitaifa kuhusu hali ya utawala na rushwa wa mwaka 2020 yameonesha asilimia 78 ya wahojiwa katika utafiti huo, wameonesha kuwa rushwa ipo kwa kiwango cha chini, na asilimia 87.7 walionesha kuwa rushwa imepungua.

Aidha, Transparency International kupitia taarifa yake kuhusu kiashiria cha rushwa mwaka 2021, ilionesha kuwa Tanzania imepata alama 39 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180, ikiwa imepanda kutoka alama 30 na nafasi ya 119 mwaka 2015.

“Kwa muktadha huo, Tanzania imeorodheshwa kati ya nchi sita zilizopiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa Afrika. Nchi nyingine ni Angola, Ethiopia, Rwanda, Ivory Coast, Senegal na Shelisheli,” alisema.

Álisema kiashiria kingine cha “The Rule of Law Index” cha “World Justice Project (WJP)” kimebainishwa kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua na kuonesha kufanya vizuri kwa mwaka wa tatu mfululizo katika kukabiliana na vitendo vya rushwa hususani, kwa kuzuia hongo, matumizi mabaya ya madaraka na ufujaji katika mihimili ya utawala, mahakama na bunge kwa kupata alama 0.46 na kushika nafasi ya 98 kati ya nchi 140 duniani.

Vilevile, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania ni nchi ya pili kwa nchi za Afrika ya Mashariki na inashika nafasi ya 12 kati ya nchi 34 za kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na juhudi za serikali katika kupambana na rushwa.

Álisema Takukuru imeendelea kuungwa mkono na kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi wakiwemo wananchi, vyombo vya habari, mamlaka, taasisi za serikali na wadau wa maendeleo.

Álisema kupitia wadau hao na wengine wengi, Takukuru ilipata fursa ya watumishi wake kujengewa uwezo, kufanya manunuzi ya vifaa mbalimbali na uboreshaji wa miundombinu ya Tehama kwa pamoja vimewezesha kuinua kiwango cha ufanisi kwenye mapambano dhidi ya rushwa.

Akizungumzia changamoto alisema kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 kulikuwa na upungufu wa majengo ya ofisi, uchakavu wa magari, na vifaa vya Tehama, uchache wa majengo ya ofisi na kutofanyika mafunzo ya kuongeza weledi kwa watumishi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Utawala na Serikali za Mitaa, Abdallah Chaurembo alisema kuwa wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.

Habari Zifananazo

Back to top button