DAR ES SALAAM: TANZANIA inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika kupunguza ukeketaji kwa asilimia 75.
Kwa sasa ipo miongoni mwa nchi zenye viwango vya nchini vya ukeketaji ikiwa na asilimia 15.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 9,2023 jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Afya, Haki za Binadamu na Maendeleo ya Jamii (HHS) wa Umoja wa Afrika, Balozi Minate Samate katika Mkutano wa Kimataifa wa kutokomeza ukeketaji chini ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Amesema, Kenya inakiwango cha wastani ikiwa na asilimia 27 wakati Uganda ina kiwango cha chini ikiwa na asilimia 1.
Nchi za Somalia, Guinea, Djibouti, na Ethiopia zimetajwa kuwa na kiwango kikubwa cha ukeketaji zikiwa na asimia 98.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2022, zimeeleza kuwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamekeketwa na asilimia 35 wamekeketwa wakiwa hawajafika umri wa mwaka mmoja
Takwimu hizo zinaeleza kuwa katika wanawake 10 basi mmoja amekeketwa.
Hata hivyo, amezitahadharisha nchi zenye viwango vya chini kuwa, utafiti unaonyesha kuwa jamii zinavuka mipaka kwenda nchi jirani kufanya ukeketaji na kuzitaka nchi kushirikiana ili kukomesha vitendo hivyo.
Kwa upande wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema sababu za ukeketaji ni Mila na Utamaduni zenye madhara kwa wanawake na watoto wake kike ambazo zimepitwa na wakati.

Amesema unyanyasaji wa kijinsia hauwezi kukubalika vijana ndio chachu ya kutokomeza Mila zilizopitwa na wakati.
” Ukeketaji unaondoa utu wa mtoto wa kike na wanawake, kila msichana anaweza kukua bila kivuli cha ukeketaji, hatuwezi kufikia dira ya maendeleo ya Tanzania 2030 ikiwa mamilioni ya wasichana wataendelea kukeketwa. ” Amesema Gwajima
Amesema, kati ya watu milioni 200 waliokeketwa duniani, asilimia 50 ni kutoka nchi za Afrika na asilimia 20 wamekeketwa na wahudumu wa afya.
” Lazima tuseme imetosha ili kulinda wanawake milioni 68 walio katika hatari ya kukeketwa,” amesema.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkaazi wa UNICEF Elke Wisch amesema ukeketaji mbali na kusababisha maumivu ya mwili na kisaikolojia inasababisha pia watoto wa kike kutotimiza malengo yao.
Nae, Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA, Mark Bryan amesema mkutano huo sio tu utaleta mabadiliko bali utagundua njia itakayomaliza ukeketaji na kutambua kiini chake.
Katika mkutano huo wa siku tatu, jumla ya nchi 21 na Mawaziri nane wameudhuria. Kauli mbiu ni mabadiliko katika kizazi kimoja kwenda kingine, kutokomeza ukeketaji.