Tanzania yataka kuwa kitovu tehama Afrika 

SERIKALI imesema imedhamiria kuiweka Tanzania katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) duniani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Jim Yonazi amesema pia serikali inataka kukuza ushawishi wake kama kitovu cha Tehama katika ukanda wa kati na kusini mwa Afrika ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayofanyika kila siku duniani kote.

Dk Yonazi alisema hayo Jumatatu kabla ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano 2022 (ITU PP22) unaofanyika Bucharest nchini Romania.

Alisema Tanzania inashiriki mkutano huo kwa sababu mahususi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inanufaika na mpango mkakati mpya wa ITU unaolenga kuleta  muunganisho wa mawasiliano kwa wote na mabadiliko endelevu ya kidijiti.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo na anatarajiwa kuwasilisha tamko la kisera la Tanzania keshokutwa.

Dk Yonazi alisema pia Tanzania itashawishi na kuvutia miradi ya kimataifa, kampuni na washirika wa maendeleo katika tehama ili kujenga uwezo na kukuza ubunifu wa vijana kutumia teknolojia zinazoibuka katika nchini.

Mkutano huo ni chombo cha juu zaidi cha kutengeneza sera cha ITU na unashirikisha wawakilishi wa nchi wanachama 193 wa umoja huo.

Katibu Mkuu wa ITU,  Houlin Zhao alisema mkutano huu utakuwa wa kihistoria.

“Nchi wananchama zitaungana katika Mkutano Mkuu wa ITU “Plenipotentiary” 2022 ili kuweka mwelekeo wa mabadiliko ya kidijitali kwa miaka ijayo, kwa manufaa ya sayari yetu na ubinadamu.” alisema Zhao alisema katika taarifa yake.

Mkutano huo unaweka sera za jumla za umoja huo, hupitisha mipango mikakati na fedha ya miaka minne na kuchagua viongozi waandamizi wa umoja, nchi wanachama wa Baraza, na wajumbe wa Bodi ya Kanuni za Redio.

Katika Mkutano huo, Tanzania inagombea kuwa katika mjumbe katika Baraza la ITU kwa kipindi cha 2023 hadi 2026. Kuna wagombea 17 wa nafasi 13 za Afrika katika Baraza hilo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button