Tanzania yataka sera rafiki fedha za kilimo

Tanzania yataka sera rafiki fedha za kilimo

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema mataifa ya Afrika yanapaswa kuweka sera rafiki za kupata fedha za kuwavuta vijana na wanawake katika kilimo ili kuharakisha mabadiliko katika mfumo wa chakula.

Dk Mpango alisema hayo jijini Kigali nchini Rwanda alipozungumza katika Jukwaa la Wakulima kwenye Mkutano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika wa mwaka 2022 (AGRF 2022).

Katika mkutano huo, Dk Mpango anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan akiwa amefuatana na viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Advertisement

Alisema Tanzania inaendelea kuchukua hatua kuimarisha sekta ya kilimo ili kuwa na uhakika wa chakula ikiwemo ajenda ya “10/30 kilimo ni biashara” inayolenga kukuza sekta hiyo kufikia asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030.

Dk Mpango alisema serikali inaendelea kuhamasisha sekta ya umma na binafsi kuwekeza katika kilimo, kuongeza bajeti ya kilimo, kutumia teknolojia ya kidijitali kwa ajili ya kupanga, kufuatilia na kutathmini huduma za ugani, masoko na malipo.

Aidha, alisema kupitia ushirikiano wa kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania imeendelea kurahisisha mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo kwa kuondoa ushuru na vikwazo vya kiforodha na visivyokuwa vya kiforodha.

Alisema ni muhimu kuweka kipaumbele katika ufadhili wa tafiti na maendeleo na huduma za ugani zitakazosaidia kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo kwa ajili ya usalama wa chakula.

Dk Mpango alisema ni muhimu ufadhili huo ukalenga uendelezaji wa rasilimali watu, kuvumbua mazao mapya pamoja na kukuza teknolojia rafiki kulingana na mazingira husika.

Alisema viongozi wa serikali na sekta binafsi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kushiriki kwenye kilimo ili wawe mfano kwa wakulima na chachu ya utengenezaji wa sera rafiki za kilimo.

Bashe jana alikaribisha mawazo kuhusu kilimo na usalama wa chakula kwa nchi za Afrika hasa Tanzania. “Nini kifanyike? Nini kiboreshwe?” aliandika katika ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter.

Alisema katika majadiliano ya PABRA (Pan Africa Bean Research Alliance) aliwaeleza Tanzania inaendelea na mpango wa kukuza uzalishaji wa maharage kutoka kwenye tani milioni 1.2 za sasa.

“Nimewaomba Taasisi ya PABRA kushirikiana na TARI, ASA na IITA katika kuongeza uzalishaji wa soya nchini Tanzania kwa ajili ya matumizi ya ndani na uhitaji wa soko la nje. Kwa sasa tuna makubaliano na China kupeleka soya tani milioni moja kwa mwaka,” aliandika Bashe.