SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), linajipanga kuomba kuandaa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) 2026.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 17 wa Shirikisho hilo uliofanyika jijini hapa jana, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema hiyo ni kutokana na kupiga hatua kwenye soka la wanawake.
“Tupo vizuri kwenye soka la wanawake, kama mnavyoona Serengeti Girls (timu ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17) imecheza Kombe la Dunia mpaka robo fainali… lakini pia Simba Queens imecheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”
“Serikali ipo kwenye marekebisho ya viwanja saba, inazidisha msukumo wa kuomba kuandaa fainali hizo za wanawake 2026 pamoja na zile za wanaume (Afcon) 2027 tayari tumejipanga na jirani zetu Kenya na Uganda tuombe kuandaa fainali hizo kwa kushirikiana.”
Alisema kwa kifupi mwaka 2022 umekuwa na mafanikio kwa uongozi wake kwani timu za taifa na klabu zimefanya vizuri.
“Mbali na Serengeti Girls na Simba Queens lakini klabu zetu Simba na Yanga zimeingia hatua ya makundi ya michuano ya CAF, tunatafuta pointi 10 ili tuingize timu nne tena kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, naamini Simba na Yanga zinaleta hizo pointi, tunajivunia maana Tanzania ni miongoni mwa nchi 12 zinazotoa timu nne kwenye mashindano, kwa mara ya tatu sasa na ninaamini hili jambo litaendelea.”
Aidha, alisema TFF ipo katika mpango wa kuhakikisha inatekeleza usimamizi mzuri wa fedha na kuongeza mapato katika mpira wa nchi hii.
Alisema ni miaka mitano mfululizo sasa TFF imekuwa ikipata hati safi na wapo katika mpango wa kuongeza wadhamini zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Mashindano ya Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
Kuhusu miradi ya Tanga na Kigamboni, Karia alisema imekamilika na itaanza rasmi kazi 2023.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, mgeni rasmi, Mohamed Abdulazizi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TFF amelitaka shirikisho hilo kuhakikisha linasambaza miradi yake katika maeneo tofautitofauti hapa nchini.
Ameipongeza pia Serikali kwa kuonesha nia ya kusaidia michezo na kuwaomba wadau kutowakatisha tamaa viongozi.