Tanzania yatoa msimamo usalama DRC

SERIKALI ya Tanzania imesema inaunga mkono jitihada za kanda kuimarisha ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema hayo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nchi za ukanda huo zinazochangia vikosi vya kijeshi katika nchi za DRC na Jamhuri ya Msumbiji.

Katika mkutano huo kwa njia ya mtandao, Dk Mpango alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kuchangia hali na mali katika misheni ya SADC nchini DRC (SAMIDRC) ili kuhakikisha kanda inatimiza malengo yake.

Advertisement

Aliipongeza DRC kwa utayari wake kutoa mchango wa ziada katika uanzishwaji wa SAMIDRC. Taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais ilieleza kuwa mkutano huo ulilenga kuangazia hali ya usalama Mashariki mwa DRC na Kaskazini mwa Jamhuri ya Msumbiji.

Mkutano huo uliridhia kuongezwa kwa muda wa vikosi vya Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) kwa miezi 12 kutoka Julai 16, mwaka huu. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera na Rais wa Msumbiji, Felipe Nyusi.

Wengine waliohudhuria ni Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe, Dk Emmerson Mnangagwa, Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, Waziri Mkuu wa Lesotho, Samuel Ntsokoane na Naibu Waziri Mkuu wa Angola, Balozi Te’te Antonio.

Katika hatua nyingine, viongozi wa nchi za Afrika wameombwa kutumia nafasi zao kusaidia kuendesha mazungumzo ya amani yatakayowezesha kumaliza mapigano yanayoendelea DRC na nchi nyingine za Afrika.

Mabalozi wa Amani kutoka nchi za Kenya na Tanzania walisema hayo katika maandamano yaliyoandaliwa na taasisi ya kidini ya Pan African Christian Foundation for Evangelization Assistance (PACFEA) yenye makao yake makuu Marekani.

Balozi wa Amani nchini Kenya kutoka Chuo cha Kimataifa cha Amani kilichopo Florida nchini Marekani, Dk Kenedy Waningu alisema mazungumzo biana ya pande mbili zinazopingana ni muhimu kumaliza vita baina ya vikundi vinavyopigana katika nchi za Afrika.

Balozi wa Amani nchini Tanzania, Mchungaji John Shusho alisema silaha si suluhisho kumaliza mgogoro na mapigano katika nchi yoyote duniani, hivyo alitoa mwito kwa makundi yanayopigana kwenye nchi za Afrika kuzungumza kumaliza tofauti zao.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *