Tanzania yavuna soko la sabuni EAC

NCHI tatu za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekuwa soko la sabuni zinazozalishwa na viwanda vikubwa vya Tanzania; amesema Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.
Mbali na nchi hizo ambazo ni Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki zinazofaidi bidhaa hizo zinazozalishwa na viwanda vikubwa vinane vya sababu Tanzania ni Malawi na Zambia.
HabariLEO Afrika Mashariki limebaini hayo wakati Naibu Waziri Kigahe akizungumzia mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Desemba 2022.
Katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri huyo alinukuu takwimu za Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Global Product Prices, kuthibitisha kuwa, bei ya bidhaa nyingi ikiwamo ya chakula ni nafuu nchini Tanzania ukilinganishwa na nchi nyingine za EAC.
“Kwa Tanzania mfumuko wa bei kwa mwezi Novemba ni asilimia 4.9; Kenya asilimia 7.38, Uganda asilimia 10.6 na Rwanda asilimia 21.7,” alisema Kigahe.
Kuhusu Tanzania kuhudumia nchi hizo kwa bidhaa ya sabuni na nyingine mbalimbali, alisema: “Nchi yetu ina jumla ya viwanda vikubwa vinane vya sabuni (ya unga na ya mche) ambavyo vinahudumia soko la ndani na pia soko la nje hasa katika nchi za Uganda, Burundi, Malawi, Zambia na DRC.”
Akaongeza: “Kiasi kikubwa cha sabuni zinazotumika hapa nchini hutengenezwa na wajasiriamali wadogo waliopata mafunzo kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) na taasisi binafsi.”
Naibu waziri huyo alisema kutokana na mahitaji ya sabuni kuwa makubwa kuliko uwezo uliopo wa uzalishaji wa ndani, sabuni zenye viwango tofauti vya ubora huagizwa kutoka nje na hivyo kumwezesha mtumiaji wa mwisho kuwa na uchaguzi wa aina ya sabuni kulingana na mahitaji yake.
“Serikali kupitia Sera ya Maendeleo ya Viwanda inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa za sabuni hususani sabuni za maji na sabuni za unga ikiwa ni pamoja na kurahisisha taratibu za uingizaji wa malighafi muhimu zinazotumika katika uzalishaji wa sabuni kutoka nje ya nchi,” alisema.