Tanzanite City mbioni kujengwa Mirerani

SERIKALI iko katika mpango wa kujenga Kituo cha Tanzanite City, kitakachojengwa Mji wa Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara,  lengo ikiwa ni kutaka madini hayo kuwanufaisha wafanyabiashara na wachimbaji wadogo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini ,Dk. Dotto Biteko, wakati wa hafla ya ununuzi wa madini ya Tanzanite, ambapo mchimbaji, Anselm Kawishe alifanikiwa kupata madini ya Tanzanite mawili ya uzito wa kilogramu 5.22,  yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 2.2 na aliyauza kwa serikali.

Dk. Biteko alisema tayari fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Tanzanite City, zimeshatolewa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba Wizara yake iko hatua za mwisho kuhakikisha ujenzi unaanza mapema.

Alisema lengo la kujengwa Tanzanite City ni kutaka madini hayo kuuzwa Mirerani na kwa kiasi kikubwa kunufaisha serikali na wananchi wanaoishi wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla.

Alisema tangu Rais Samia aingie madarakani, makusanyo ya kodi ya serikali kwa madini ya Tanzanite yameongezeka, kutoka Sh bilioni 475 hadi Sh bilioni 625 kwa mwaka.

Alisema sekta ya madini imepanda katika ukusanyaji kutoka asilimia tano hadi kufika asilimia saba na kufanya uuzwaji wa madini nje ya nchi kuwa mzuri na wenye tija wwa serikali.

Akizungumza juu ya uuzwaji wa madini ya Tanzanite vipande viwili kwa serikali, Waziri Biteko alisema uamuzi wa kuuza madini hayo umefanywa na Kawishe mwenyewe kwa kuwa na imani na serikali yake na sio vinginevyo.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru alisema wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2022/23, imejipanga kukusanya mapato ya zaidi ya Sh Bilioni 822.

Naye Kawishe akizungumza bàada ya kusaini mkataba wa mauziano na serikali uliosainiwa na Gavana wa Benki Kuu, Prof. Florens Luoga kwa niaba ya Wizara ya Fedha, alisema amechimba madini Kwa zaidi ya miaka 15 bila mafanikio, lakini anashukuru kwa hatua aliyofikia hivi sasa na atashirikiana na serikali kwa kila hali.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button