Tari, AMDT na ubia kuongeza uzalishaji mbegu bora za alizeti

“ SISI kama TARI (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania), tumeona ni vema kushirikiana na wadau kuweka ubia kati ya serikali na sekta binafsi hasa katika uzalishaji wa mbegu.” Meneja Mradi wa Ubia kati ya Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT), Frank Reuben anasema hayo anapozungumza na ugeni wa watumishi 16 waliotembelea taasisi hiyo katika Kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa, Morogoro.

Reuben ambaye pia ni Mratibu wa Utafiti wa Zao la Alizeti Kitaifa, anasema kwa kushirikiana na sekta binafsi, teknolojia wanazozalisha zitawafikia haraka wakulima na wasindikaji.

Anasema katika zao la alizeti, Tari Ilonga imekuwa ikitafuta fedha na kuzitoa kwa kampuni mbalimbali ili zizalishe mbegu bora na kuziuza kwa wakulima kama ruzuku. “Tunapopata fedha, tunabaki na kiasi kidogo kufanyia ufuatiliaji kuona kama kampuni zilizopata fedha zinazalisha.

Advertisement

Nyingine zinachangia kidogo kwenye uzalishaji wa mbegu za daraja la awali ambazo kampuni haizihitaji,” anasema. Kwa mujibu wa Reuben, kampuni zinazowezeshwa kuzalisha mbegu, hupata utaalamu kutoka Tari hasa namna bora ya kuzalisha mbegu.

“Uzalishaji wa mbegu ni jambo la kisayansi kwani kuna hatua za kisayansi zinazopaswa kufuatwa na kuna kanuni za uzalishaji bora wa alizeti. Ili kuhakikisha nchi inapata mbegu za kutosha, zinazozalishwa hupatikana kwa bei rahisi na mbegu hizi huongeza usalama wa mbegu,” anasema. Reuben anasema pamoja na mradi kuelekeza uzalishaji wa mbegu, katika siku zijazo wataangalia pia na kundi la wamiliki wa maduka ya pembejeo ili wahusishwe kumsaidia mkulima.

“Fedha tunazopata sisi zinakuwa za serikali kwa hiyo tunapoipa fedha kampuni, inabidi ifuate masharti ya serikali,” anasema. Kwa mujibu wa meneja na mratibu huyo, ujio huo wa watumishi 16 wa AMDT katika kituo cha Tari- Ilonga, mapema mwezi uliopita ni udhihirisho kuwa wameridhishwa na kazi zinazofanywa na taasisi hiyo ya kilimo hivyo wanataka kuimarisha zaidi ubia uliopo.

“Waliangalia na kujikita zaidi katika uzalishaji wa mbegu na wakabaini mbegu za alizeti zina mnyororo mkubwa unaohitaji wadau wengi,” alisema. Wataalamu wanasema mbegu za zao hilo zina madaraja mengi yakiwemo ya awali, msingi na yanayothibitishwa ubora.

“Lakini kuna mbegu zinazalishwa na wakulima zikiangaliwa zote hizo unakuta alizeti ina mnyororo mkubwa katika kipengele cha Watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Kituo cha Ilonga, Kilosa mkoani Morogoro wakiwa na watumishi kutoka Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) waliotembelea kituo hicho cha Tari hivi karibuni. mbegu,” anasema Reuben.

Anakiri miaka mingi iliyopita uendelezaji wa alizeti haukuwa mkubwa lakini sasa, serikali imeamua kuwekeza na kulifanya zao hilo kuwa la kipaumbele. Mkurugenzi wa Kituo cha TariIlonga, Emmanuel Chilagani anafurahia ujio wa watumishi hao wa AMDT kituoni kwake akisema kilimo kwa kushirikiana na wadau kunasaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu bora.

“Alizeti ni miongoni mwa mazao matano ya kimkakati katika kituo chetu,” anasema Chilagani. Anayataja mazao mengine kuwa ni mahindi, mazao jamii ya mikunde, uwele na ulezi. Chilagani anasema wanaendelea na juhudi katika tafiti zinazolenga kuongeza thamani kwenye mazao hayo. “Kwa sasa kituo kinategemea mvua katika uboreshaji wa mbegu; huu si mfumo mzuri sana kwa sababu tunazalisha mara moja kwa msimu.

Tukipata mfumo mzuri kupitia serikali na wadau kwa mwaka tunaweza kuzalisha zaidi ya mara moja na pia itasaidia upatikanaji wa mbegu na kuepusha hasara maana tumewekeza kwenye uzalishaji,” anasema Chilagani. “Niwaombe AMDT tuendelee kushirikiana zaidi kwani tunayo mengi ya kushirikiana ili tuboreshe mfuko wa uzalishaji wa alizeti,” anasema.

Naye Mtendaji Mkuu wa AMDT, Charles Ogutu anasema wanauchukulia ubia kati ya AMDT na TariIlonga kama sehemu ya usalama wa mbegu kwani unachangia kuwa na usalama wa mbegu kitaifa. Ogutu anasema kama taifa wanatambua upungufu mkubwa uliopo wa mafuta ya kula hivyo wanachangia katika programu hiyo ya kuwezesha uzalishaji wa mbegu bora za kutosha.

Akizungumzia namna taasisi yake inavyochangia kutatua tatizo hilo la upungufu wa mafuta ya kula, Ogutu anasema: “Mbegu zinapozalishwa na hasa zilizothibitishwa zinapotoka na kumfikia mkulima, uzalishaji huwa wa tija zaidi.” JADIDAAA “Kwa namna nyingine tunaweza kusema kuwa, kwa ubia huu tunawasaidia Watanzania wengi ambao pamoja na kuongeza uzalishaji, pia wakulima wanaongeza kipato kwa kiasi kikubwa.”

“Kipato kikiongezeka watu wengi wanapata ajira maana uzalishaji unakuwa mkubwa na viwanda vinavyosindika zao la alizeti vinaongezeka na kuongeza uzalishaji na pia vinaweza kusindika kwa muda mrefu zaidi kuliko awali kwa sababu alizeti itakuwa inapatikana kwa wingi zaidi,” anasema Ogutu.

Anaeleza kuwa mchango wa ubia wao kati ya AMDT na Tari umeongeza upatikanaji wa mbegu moja kwa moja kwa mkulima. Ogutu anasema katika msimu uliopita kupitia ubia wao, waliwezesha sekta binafsi kuzalisha tani 40 kwa mwaka na katika msimu huu, wanategemea si chini ya tani 100. “Tani 100 ina maana tumeongeza zaidi ya asilimia 100 ndani mwaka mmoja.

Tunategemea ubia huu utaendelea kuchochea sekta binafsi kuzalisha mbegu zaidi ili kuwafikia wakulima,” anasema Ogutu. Anasema wanawawezesha Tari ambayo nayo huwezesha kampuni inazoingia nazo mkataba kuzalisha mbegu hali inayozifanya kampuni hizo kuongeza kipato katika biashara zao. Ogutu anasema kupitia mkakati baina yao na Tari, wataongeza uzalishaji. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Tanzania ni mzalishaji namba mbili katika Afrika na mzalishaji namba 10 duniani kwa alizeti.

“Tunaamini ubia huu ni muhimu kuongeza uzalishaji ambao pia unalenga kumwongezea mkulima kipato. Tunategemea ubia huu utaendelea na msimu unaofuata na tutaangalia maeneo mengine ambapo tutaweza kushirikiana hata ikiwezekana kuzalisha mbegu mara mbili au tatu kwa mwaka,” anasema.

Kumekuwepo na jitihada za makusudi za serikali chini ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuongeza uzalishaji wa michikichi na alizeti kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kula. Kutekelezwa kwa lengo la alizeti kuwa zao la kimkakati kutasaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 650,000 na uzalishaji wa ndani ni tani 290,000. Alizeti huchangia asilimia 83 ya mafuta ya kula yanayozalishwa nchini. Asilimia nyingine 17 huzalishwa kutokana na mazao ya michikichi, pamba, minazi, karanga, khatam na mengineyo.

Tari kwa kushirikiana na wadau imetoa teknolojia mbalimbali ikiwemo ya mbegu bora zikiwamo aina ya Record, TARI-ILO 2019 na TARI-NAL 2019. Wadau wanaonesha imani yao wakisema mradi huo kati ya AMDT na Tari-Ilonga utachochea zaidi uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima nchini.

Waziri Hussein Bashe mara nyingi hukaribisha sekta binafsi kuzalisha mbegu za alizeti kukabiliana na uhaba wa mbegu. Tari-Ilonga imeanza kutekeleza kwa vitendo kauli hiyo kwa kushirikiana na kampuni za mbegu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *