Tari ilivyodhibiti mateso ya tembo wa mkonge kwa wakulima

“KUNA mdudu Tembo wa Mkonge huyu anatusumbua sana wakulima wa mkonge. Tunapuliza dawa lakini wanasumbua sana hivyo tunapambana.”

Mkulima wa mkonge katika eneo la Kilimongwido wilayani Pangani mkoani Tanga, Aisiani Mero anaeleza changamoto wanayokabiliana nayo katika kilimo cha mkonge.

Mero aliyeanza kilimo hicho mwaka 2020/2021, ana shamba la ukubwa wa ekari 500 na kwa maelezo yake bado hajaanza kuvuna anatarajia kuvuna mwishoni mwa mwaka huu.

Changamoto nyingine anayoizungumzia ni magonjwa pamoja na wanyama waharibifu wa zao hilo kama ngedere, tumbili, nyani, ngiri na nguruwe pori.

Naye mkulima wa Kijiji cha Kibaranga wilayani Muheza mkoani Tanga, Salim Ramadhan anasema Tembo wa Mkonge ni mdudu mharibifu sana na anaiomba serikali iwasaidie dawa kumtokomeza. Ramadhan ana shamba la ekari 15 na sasa ni miaka miwili tangu aanze kilimo hicho.

“Pia nguruwe wanaingia kwenye shamba wanakwanyua mkonge wa katikati na kuula kama miwa,” anasema. Katika kutafuta suluhisho, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imefanikiwa kumdhibiti mdudu huyo kwa kufanya utafiti kwa miaka mitatu sasa na inajiandaa kusambaza teknolojia hiyo kwa wakulima wa mkonge nchini baada ya majaribio kufanikiwa.

Mtafiti wa Tari Kituo cha Mlingano Tanga, Dk Mgaya Maumba anasema changamoto kubwa iliyokuwa inawasumbua ni Tembo wa Mkonge lakini tayari wamefanya utafiti kumdhibiti.

“Katika miaka mitatu hii ambapo ndani ya kituo tumefanya majaribio na mwaka uliopita tumeweza kutoka nje ya kituo kwenda kufanya majaribio kwa baadhi ya mashamba ya wakulima, matokeo yanaonesha karibia asilimia 90 ni mazuri.

“Kwa hiyo tunakamilisha taratibu tuweze kuifanya hii teknolojia sasa iwe rasmi. Huyu mdudu ni mwaribifu sana, anakula katikati ya kiini kichanga majani yanapokua kwa hiyo majani yakiwa yanazaliwa yanatoka tayari yakiwa yameathirika huwezi kupata nyuzi nzuri za daraja la kwanza au la pili na wakati mwingine mkonge unakufa kabisa,” anasema Dk Maumba.

Anasema changamoto nyingine anayoizungumzia ambayo imepatiwa ufumbuzi ni kuwafikishia wakulima mbegu ya zao hilo katika maeneo waliyopo.

“Wakulima walilalamika umbali wa kusafirisha mbegu kutoka maeneo tunayozalisha, lakini Tari Mlingano tumejipanga sasa tutazalisha mbegu kwenye maeneo ya wakulima, hata hivyo serikali imeshazipa nguvu baadhi ya halmashauri ambazo zinazalisha mbegu kwa kiwango kidogo tunategemea Tari ifikie walau kila mkoa unaolima mkonge kuzalisha mbegu karibu na wakulima,” anasema. Dk Maumba

Anasema hivi sasa Tari Mlingano wamekuwa na miaka zaidi ya mitatu ya uzalishaji wa mbegu bora za miche ya mkonge. Na katika kipindi hicho cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2020/2021 mpaka 2022/2023 kituo hicho kimekuwa na mapinduzi makubwa katika uzalishaji wa mbegu za mkonge ambao utaleta mapinduzi makubwa katika hitaji la dunia la upatikanaji wa nyuzi za mkonge.

“Tangu mwaka 2020/2021 mpaka 2022/2023 Tari Mlingano wamezalisha miche karibia milioni 12 ambapo mpaka mwaka huu Juni 30 takribani miche milioni 7.5 imeshasambazwa kwa wakulima. Kwa miche hiyo milioni 7.5 ni sawa na ekari 4,687.5 (hekta 1,875) zinazopandwa,” anasema.

Kwa maelezo ya Dk Maumba, kwa mbegu hiyo bora wanategemea wakulima wakifuata kanuni bora za kilimo cha mkonge kama walivyoelekezwa, mavuno kwa hekta moja itakuwa ni wastani wa nyuzi za mkonge tani tatu kwa mwaka.

“Sasa kwa hekta hizi 1,875 katika mavuno ya wastani wa tani tatu kwa kila hekta, tunategemea jumla ya tani 5,625 zitakuwa zimevunwa ifikapo mwishoni mwa 2024/2025, ambazo kwa uchache tukichukulia kwa soko la ndani daraja la katikati kwa bei ya wastani ya ndani ya nchi kwa tani moja ni milioni nne.

“Kwa hiyo kwa hizi tani ambazo zinatarajiwa kwenda kuvunwa (5,625) tunategemea tutaingiza fedha ya Kitanzania baada ya muda huo karibia shilingi bilioni 22.5 ambazo ni sawa na Dola za Marekani milioni 9.2. Ukiangalia fedha hizi mgawanyiko wa wakulima ambao wamechukua hizi mbegu ni takribani wakulima 600,” anasema Dk Maumba.

Anasema mkonge ni zao la kimkakati lakini pia la kibiashara linalosafirishwa nje ya nchi hivyo kwa uzalishaji wa miche ambayo serikali imesaidia mategemeo ni mapato ya fedha za kigeni kuongezeka.

“Mahitaji ya Tanzania lengo tulilojiwekea ni kuzalisha tani 120,000 kwa mwaka ambapo kwa sasa bado tupo nyuma mpaka itakapofika Desemba mwaka huu (2023) tunatarajia labda zitafika tani 60 kwa hiyo tutakuwa nusu ya mahitaji ya kuzalisha kwa mwaka,” anasema.

Mkurugenzi Mkuu wa Tari, Dk Geofrey Mkamilo anasema taasisi hiyo imekuwa ikionesha na kutoa elimu kuhusu teknolojia mbalimbali za kilimo iliyonazo. Huwaonesha na kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zilizopo katika kilimo kwa kuwashauri wawekeze wapi, zao gani na watumie teknolojia ipi katika mnyororo mzima wa thamani katika kilimo.

“Tari tuna teknolojia zilizopo kwenye mazao ya kimkakati na mengineyo kama alizeti, ngano, mkonge, mchikichi, korosho, pamba na mengineyo,” anasema Dk Mkamilo. Tari inafanya kazi kwa mtandao wa vituo 17 vya utafiti wa kilimo nchini katika ikolojia mbalimbali.

Juni 21, 2021 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema serikali imedhamiria kufufua mkonge nchini na kuwataka Watanzania wachangamkie fursa hiyo kwa kujenga viwanda vya kuchakata bidhaa zitokanazo na zao hilo kama sukari, dawa, vinywaji, mbolea na nyuzi.

“Mkonge ni utajiri, ni fedha ya uhakika na ni zao ambalo mzazi akiwekeza kwa ajili ya mtoto wake, litamsaidia baadaye hata kama yuko darasa la saba, mkonge atakaoupanda leo utamsomesha hadi chuo kikuu,” alisema Majaliwa. Anasema mkulima wa kawaida anaweza kuanza kulima hata ekari moja, ambayo atapanda miche 1,600 na baada ya miaka mitatu atavuna tani moja na nusu hadi mbili iwapo shamba litasimamiwa vizuri. Bei ya tani moja ya mkonge wa daraja la juu ni Sh milioni nne.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button